KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imelieleza Bunge kuwa Katika kipindi cha miaka mitatu TIC kimesajili miradi 757 inayokadiriwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 9.
35.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, David Kihenzile akiwasilisha bungeni, taarifa ya kamati hiyo leo Februari Mosi, 2023 amesema miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira ajira 111,332.
Amesema, kati ya miradi hiyo asilimia 31 inamilikiwa na Watanzania, 41 inamilikiwa na wageni na asilimia 28 ni ya ubia kati ya Watanzania na Wageni.
Kihenzile amesema, serikali inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara na Uwekezaji Nchini.
“Katika kipindi cha mwaka 2021/2022 Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) imesajili miradi 54 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 238.24.”:Amesema
Amesema kuanzia mwaka 2017 hadi 2022 miradi katika sekta ya viwanda vya uzalishaji ilitarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 16,535 na ajira nyingi zisizo za moja kwa moja katika mnyororo wa usambazaji.
Aidha, amesema pamoja na mafanikio hayo kamati ilibaini changamoto kadhaa katika sekta ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kukosa vivutio vya kikodi kwenye programu ya EPZA ambavyo awali vilipatikana hivyo kusababisha baadhi ya wawekezaji kufuta usajili wa miradi ikiwa ni pamoja na kutokuridhiwa kwa Sera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi hivyo kusababisha wawekezaji katika pogramu ya EPZA kutofaidika na vivutio.