Ajitolea nyumba yake iwe kituo cha polisi

MWANZA:  Mfanyabiashara na mkazi wa Kata ya Ilangala, Kisiwa cha Gana, Wilaya ya Ukerewe, Nyamitere Ugunya,  amejitolea nyumba yake aliyokuwa anaitumia na kuikabidhi kwa Jeshi la Polisi ili iwe kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa huduma za usalama kwa wakazi zaidi ya 6,000 wa kisiwa hicho.

Nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya 15 inatakiwa kufanyiwa ukarabati mdogo wa kuwekewa miundombinu na mifumo ya majitaka itakayokidhi hadhi ya kituo cha polisi.

Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbrod Mutafungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo kunaenda kutatua changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikiwakabili kisiwani hapo.

Pia kamnda  amemuomba mfanyabiashara huyo aliyejitolea kujenga kituo cha polisi kukamilisha mapema hadi ifikapo mwishoni mwa Januari 2024.

Hata hivyo, wakazi wa Kisiwa hicho wamemweleza Kamanda Mutafungwa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na kuomba Serikali iwatatulie ikiwa ni kukithiri kwa vitendo vya mmonyoko wa maadili, ulevi, utovu wa nidhamu, wizi wa nyavu na injini za mitumbwi, uvuvi haramu, ukatili wa kijinsia, udokozi, mauaji, unyanyasaji na ukosefu wa alama za mipaka ziwani zinazoonyesha mpaka wa Tanzania na Uganda.

Aidha, wananchi hao wameliomba Jeshi la Polisi kusaidia kukamilisha mapema ujenzi wa kituo hicho ili changamoto hizo zitatuliwe huku wakiomba mipaka inayotenganisha Tanzania na Uganda iwekwe ziwani ili kupunguza matukio ya wavuvi wa pande hizo mbili kuingiliana.

Habari Zifananazo

Back to top button