NEW DELHI, INDIA; BAADA ya kusubiriwa kwa muda mrefu na wapenzi wa filamu za mapigano duniani kote, hatimaye waigizaji wawili nguli kutoka Bollywood nchini India Akshay Kumar na Tiger Shroff leo Machi 26 wanazindua filamu yao ya Bade Miyan Chote Miyan inayopinga ugaidi.
Filamu hiyo ya kihindi baada ya kuzinduliwa leo, Aprili 10, 2024 itapelekwa katika kumbi za sinema kwa ajili ya uzinduzi mwingine, lugha zilizotumika katika tafsiri ya filamu hiyo ni Kihindi, Kitamil, Kitelugu, Kimalayalam na Kikannada.
Katika Bade Miyan Chote Miyan, kiongozi wa magaidi Prithviraj Sukumaran, ameteka nyara silaha ya maangamizi, ambayo ni hatari sana kwa usalama wa India, hivyo India inaamua kuwatuma wanajeshi wake, ili wakairudishe silaha hiyo iliyotekwa na magaidi.
Jukumu hilo wanapewa wanajeshi Akshay na Tiger wakiongoza kikosi cha uokoaji wanaokwenda kwa ajili ya kurudi na silaha hiyo, sasa utamu wa filamu hiyo ni mtiririko wa visa vya matukio yaliyopangika barabara yanayoamsha hamasa na kujenga hofu kwa mtazamaji wa filamu hiyo.
Filamu hiyo imeongozwa na Ali Abbas Zafar, ambaye hapo awali ameongoza filamu ya Sultan na Tiger Zinda Hai.
Filamu hiyo imetayarishwa na Kampuni ya Pooja Entertainment na AAZ Films na inasambazwa na kampuni mbili Yash Raj Films na PVR Inox Pictures.
Kwa wasioijua filamu hii ya Bade Miyan Chote Miyan, filamu ya awali ilitolewa mwaka 1998 ambapo iliigizwa na mkongwe wa filamu za Bollywood Amitabh Bachchan na Govinda na muongozaji wake alikuwa David Dhawan.
Imetayarishwa na Festo Polea