Akutwa na misalaba 14 iliyong’olewa makaburini

POLISI mkoani Morogoro inamshikilia fundi seremala, Meshack Azikam (23) mkazi wa Kata ya Kichangani,Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma ya kukutwa na misalaba 14 ya chuma iliyong’olewa kutoka katika makaburi ya Kola yaliyopo Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kujinufaisha kiuchumi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Alex Mkama amesema leo Juni 26, 2023 kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa jana usiku, baada ya kupokea taarifa ya wizi wa misalaba ya chuma katika makaburi hayo.
“ Tumekuwa tukipokea taarifa ya changamoto ya wizi wa misalaba hasa kwa madhehebu ya Kikristu, wamekuja kulalamika na tumefanya ufuatiliaji, “ alisema Mkama na kuongeza kuwa:
“ Katika ufuatiliaji wetu tulifanikiwa kumkamata mtu mmoja anaitwa Meshack Azikam (23) fundi seremala mkazi wa Kichangani , Manispaa ya Morogoro ni baada ya kuweka mtego kwenye makaburi ya Kola na tukamkamata akiiba msalaba mmoja,” amesema Kamanda Mkama.
Amesema baada ya kukamatwa na msalaba huo mmoja akiwa makaburini hapo na alienda kupekuliwa nyumbani kwake na alikutwa akiwa na misalaba 14 nyumbani kwake.
“ Mtuhumiwa huyo baada ya kuiba misalaba hiyo anachokifanya ni kuondoa majina ya marehemu na kuipaka upya rangi na kuiuza tena na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote ule, “ alisema Kamanda Mkama.
Wakizungumzia tukio la wizi wa misalaba katika makaburi ya Kola, muumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Morogoro usharika wa Mji Mpya , Pascal Mataba ,alisema kuwa suala la wizi wa misalaba inayong’olewa inaonesha wazi watu wamefikia mahali hawana hofu ya Mungu .
Mratibu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice la Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro , Cosmas Kigona alisema msalaba unapowekwa katika kaburi ni alama ya utambulisho wa marehemu kwa ndugu zake wanapokuwa na shughuli maalumu za kiibada na kuzuru kaburi lake ,hivyo inapong’olewa ni kupoteza alama ya mtu huyo alipozikwa.