Alex Jela miaka 12 kujifanya Askari Upelelezi

SIMIYU: MAHAKAMA ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imemhukumu Alex Nangale (24) mkazi wa Mtaa wa Sokoni mjini Maswa wilayani humo kwenda jela miaka 12 baada ya kukutwa na hatia kwa makosa 8 likiwemo la kujifanya Askari Polisi kitengo cha upelelezi.

Hukumu hiyo imetolewa jana Mei 30, 2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo,Enos Misana katika kesi ya jinai namba 45 ya mwaka 2023 baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka mahakamani hapo na kuthibitisha alitenda makosa hayo.

Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo mahakamani hapo, Mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya hiyo, Mkaguzi msaidizi, Vedastus Wajanga alieleza kuwa Mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa nane.

Mwendesha Mashitaka huyo alisema kuwa Machi 7,2023 katika Mtaa wa Sokoni mjini Maswa, mshitakiwa alijitambulisha kwa jina la Amos Malimi na kuwa ni Askari Polisi na yupo kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai na kuanzia hapo hadi Machi 31,2023 alikuwa akiomba pesa kutoka kwa Muhanga (jina linahifadhiwa) kwa kutumia utambulisho huo na kujipatia kiasi cha fedha Sh milioni 1,740,000.

Katika kosa la kwanza Mwendesha Mashitaka alielezea mahakama kuwa mshitakiwa alijifanya Askari Polisi kinyume na kifungu cha 369 (1) (2) huku makosa saba yote yakiwa ni kujipatia fedha kwa njia udanganyifu kinyume cha kifungu 302 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2022.

Jumla ya mashahidi wanne na vielelezo vinne vilitolewa na upande wa mashtaka mahakamani hapo, huku upande wa mashitaka ukiomba kutolewa kwa adhabu kali kwa mshitakiwa kwani makosa aliyotenda yamechafua taswira ya taasisi ambayo ni jeshi la polisi.

Baada ya Mahakama kumkuta na hatia mshitakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwani ni mkosaji wa mara ya kwanza na anafamilia inamtegemea.

Hatahivyo baada ya utetezi wake Mahakama hiyo ilimhukumu adhabu ya miaka mitano jela kwa kosa la kujifanya Askari Polisi na Miaka saba kwa makosa saba ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakiwa kulipa fidia ya Sh 1,740,000/-kwa Muhanga.

Habari Zifananazo

Back to top button