Aliyebaka na kumuua binti kufia gerezani

MAHAKAMA ya Rufaa imetupa rufani iliyowasilishwa na mkazi wa Mkoa wa Mara, Matiko Chandruku ya kupinga kutiwa hatiani na kuhukumiwa kifo kwa tuhuma za kumbaka hadi kumuua binti wa miaka saba.

Uamuzi huo ulitolewa mbele ya jopo la majaji watatu; Gerald Ndika, Winfrida Korosso na Othman Makungu baada ya kukubaliana na adhabu ya kifo kwa mrufani huyo, iliyotolewa na Mahakama Kuu Musoma.

“Mahakama inaridhika kwamba mashitaka dhidi ya mrufani yalithibitika pasipo kuacha shaka na kwamba mahakama ilikuwa sahihi kutoa hukumu ya kifo kwa mrufani hasa ikizingatiwa kwamba wakati akitenda kosa hilo alikuwa ametimiza miaka 18,” ilisema sehemu ya hukumu hiyo.

Wakati wa kusikilizwa rufaa hiyo, mrufani alidai maelezo ya onyo yaliyowasilishwa wakati wa kusikilizwa kesi Mahakama Kuu yalipokelewa kimakosa kama kielelezo cha ushahidi na alihukumiwa kimakosa hukumu ya kifo kwa sababu wakati huo hakuwa ametimiza miaka 18.

Katika hukumu iliyotolewa Mahakama ya Musoma, jaji alisema mrufani aliibua hoja ya maelezo ya onyo wakati wa rufaa kama sehemu ya kujitetea.

Mahakama ya Rufaa ilibaini kutoka katika ushahidi kwamba maelezo ya onyo yalipowasilishwa mahakamani na kupokelewa kama kielelezo cha ushahidi mrufani hakupinga na pia mahakama ilibaini kuwa yalirekodiwa katika Kituo cha Polisi ndani ya muda.

Walisema kama mrufani alikuwa na hoja kuhusu kielelezo hicho angepinga wakati kinatolewa na upande wa mashtaka ungepaswa kutolea maelezo lakini hicho hakikufanyika, hali ambayo inaonesha mrufani alikubaliana na maelezo hayo ambayo ndani yake alionekana kukiri kumuua binti huyo.

Ilidaiwa katika mkasa husika kwamba Juni 30, 2018, saa mbili usiku mwanamke aliyetajwa kwa jina la Lucia Ricardo aligundua binti yake wa miaka saba hakuwepo nyumbani ndipo alipoamua kushirikisha ndugu na kuanza kumtafuta bila mafanikio.

Walitoa taarifa kwa mjumbe na Mwenyekiti wa Kijiji ambao waliwashauri wakalale kwa kuwa ilikuwa ni usiku.

Kazi ya kumtafuta iliendelea asubuhi kwa ushirikiano na wanakijiji wengine, baada ya saa kadhaa taarifa zilipatikana kwamba binti huyo alionekana mara ya mwisho akiwa na mrufani na kaka yake.

Iliendelea kudaiwa kuwa wanakijiji waliwakamata mrufani na kaka yake lakini wakiwa njiani kuelekea ofisi za serikali ya kijiji, kaka yake alitoroka.

Katika ofisi za Serikali ya Kijiji mrufani alihojiwa na kukiri kwamba alimuua binti na kumficha katika eneo la kilima cha Ujerumani, taarifa zilifikishwa polisi na walipofika mrufani aliwaelekeza alipomficha na kuukuta mwili.

Baada ya uchunguzi ilidaiwa binti huyo alikufa kwa kukosa hewa wakati wa purukushani hizo huku mwili wake ukiwa na viashiria vya kubakwa.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button