Aliyehamisha mto apewa siku 7 kuurejesha

KATAVI: Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Jamila Yusuf ametoa siku saba kwa mwekezaji wa machimbo ya madini aina ya dhahabu ,Anseimo Mjinga, aliyehamisha mto uliopo Kijiji cha Mtisi Kata ya Sitalike kusimamisha shughuli zake mara moja na kuurudisha mto huo.

Ametoa agizo hilo alipokuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kijiji cha Mtisi ambao wameulalamikia uongozi wa kijiji hicho kutoa eneo linalopakana na mto kumpa mwekezaji ambaye amehamisha mto kutoka eneo lake la asili na kuuchepusha.

Aidha ametoa onyo kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mtisi kwa kushindwa kuchukua hatua mapema kabla ya mwekezaji  hajafanya uharibifu katika mto huo,na kumtaka Mkurugenzi  Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ,Nsimbo Mohamed Ramadhan kumchukulia hatua za kisheria mwekezaji huyo pamoja na wote walio husika.

Katika hatua nyingine ameagiza idara zinazo husika na mazingira ndani ya wiki mbili ziwe zimetembelea maeneo yote ambayo viwanda vya kuchenjua madini maarufu kama plant ili kufanya tathimini ya usalama wa kimazingira na binadamu kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya Nsimbo Privatus Aloyce amesema mwekezaji huyo amekiuka sheria ya mazingira katika vyanzo vya maji ambayo inataka shughuli zozote za kibinadamu ikiwemo uwekezaji kufanyika umbali wa mita 60 kutoka kingo za maji au chanzo cha mto.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button