Aliyehukumiwa miaka 30 jela kwa ubakaji aachiwa
ALIYEDAIWA kumbaka mwanamke wa miaka 58 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Joseph Mathias amefutiwa hatia na kifungo hicho baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Tabora kubaini hati ya mashitaka ilikuwa na kasoro.
Licha ya Mathias kutumikia kifungo cha miaka minane jela, aliachiwa huru jana baada ya mahakama hiyo kukubali rufani yake iliyoambatana na maombi mawili kwamba hati ya mashitaka ilikuwa na kasoro na pia kitendo cha yeye kukiri kosa kilikuwa sahihi.
Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Mfawidhi Kanda hiyo, Athuman Matuma alisema kuwa wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo, pande zote mbili ikiwemo Mawakili wa Serikali, Robert Kumwembe na Nurdini Mmary walikubaliana na rufaa kwamba hukumu iliyotolewa haikuwa sahihi kutokana na mshitakiwa kukiri mashitaka yenye kasoro.
Walidai kuwa mrufani alishitakiwa chini ya kifungu cha 130 (2) (a) cha Kanuni ya Adhabu bila kutaja masharti ya kifungu cha 130(1) ambacho kinaunda kosa hilo.
Pia walidai mrufani hakukubali kosa bali kifungu 130 (2) (a) ambacho kinafafanua tu mojawapo ya vipengele vya ubakaji.
Kumwembe alidai kuwa mrufani katika kesi hiyo anayo haki ya kukata rufaa kwa sababu alikiri kosa katika mashitaka ambayo hayakutajwa na kifungu hicho.
Wakili huyo alidai kwamba mashitaka hayo pia hayakutaja kifungu maalumu ambacho kinaelezea kuhusu adhabu ikiwa mshitakiwa atatiwa hatiani.
“Kutokana na hali hiyo, mawakili wa serikali waliitaka mahakama hii kuruhusu rufaa hii kwa kufuta hatia na kuweka kando adhabu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya. Pia waliiomba mahakama kuagiza mrufani kusikilizwa upya kwa sababu ametumikia miaka minane kati ya miaka 30,” alisema Jaji Matuma.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo alidai kuwa yuko tayari shauri hilo kusikilizwa upya.
Jaji Matuma alisema: “Nakubaliana na rufaa hii na kufuta hatia na kifungo cha miaka 30 kwa mrufani,” alisema.
Pia alisema licha ya pande zote kuomba kusikilizwa upya kwa shauri hilo, hakubaliani na hoja hizo kwa sababu hawawezi kurudia mashitaka yenye kasoro.
Alisema: “Ningemwacha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kutumia busara yake kama kumshitaki tena mrufani au la, lakini naona kwamba mrufani tayari ametumikia kifungo cha miaka minane lakini pia mwathirika alikuwa na umri wa miaka 58 wakati tukio hilo linatokea na mpaka sasa ni mzee wa miaka 66 na inaweza kumkumbusha mateso aliyofanyiwa miaka minane iliyopita.”
Alisisitiza kuwa iwapo mrufani alitenda kosa hilo, miaka minane aliyoitumia gerezani inamtosha kwa madhumuni ya kutomruhusu DPP kumshitaki upya Mathias.
Mathias alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nzega akidaiwa Novemba 24, 2016 saa 6 usiku kwenye Kijiji cha Mwashina Wilaya ya Nzega, alimbaka Christina Evarist mwenye umri wa miaka 58.
Mshitakiwa alidaiwa kukiri makosa hayo na kukubali maelezo ya awali na hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.