Aliyeiba fedha za marehemu alipa faini, aikwepa jela

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Makalaghe Shekhalaghe kulipa faini Sh  7,000,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya mahakama hiyo kumkuta na hatia ya kuiba Sh 198,750,000 kutoka katika akaunti ya marehemu mume wake.

Pia mahakama hiyo imeamuru kuchukuliwa nyumba ya Makalaghe iliyopo Msamvu mkoani Morogoro na kuingizwa katika mirathi namba 23 ya mwaka 2022.

Hukumu hiyo imesomwa juzi  na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.

Advertisement

Akisoma hukumu hiyo Kabate alisema katika hukumu hiyo mahakama imeegemea katika kifungu cha 258 na 265 vya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alisema vifungu hivyo vinaeleza wazi wizi ni nini na mazingira gani ambayo ya yanatafsiriwa kama wizi.

Kabate alisema pia ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashitaka umeeleza jinsi ambavyo fedha ilikuwa ikitolewa benki na mshitakiwa baada ya kifo cha mume wake.

Alisema pia mshitakiwa mwenyewe alikiri kutoa na kutumia fedha kwa matumizi binafsi na kutoa sadaka katika masjid Huddah mkoani Lindi.

Kabate alisema kwa kukiri kwake na ushahidi wa taarifa za kibenki mahakama haina maswali ya ziada ya kujiuliza juu ya ukweli kuwa mtuhumiwa aliiba kiasi hicho cha fedha.

Alisema kutokana na utetezi wa mshitakiwa alioutoa kabla ya hukumu kuwa sehemu ya fedha alizoiba alizitoa kama sadaka katika masjidi na shahidi wake alieleza jinsi ambavyo walinufaika na msaada huo mahakama imeona impunguzie adhabu.

Pia mahakama imeshawishika na hoja za wakili wa utetezi alioutoa kupitia kifungu cha 27 kifungu kidogo cha pili kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo 2022.

Alisema pia mahakama hiyo haina kumbukumbu za makosa ya nyuma pia mshitakiwa ana familia inayomtegemea hivyo mahakama hiyo inamuhukumu kulipa faini ya Sh  7,000,000 au kifungo cha mwaka mmoja pamoja na kukabidhi nyumba yake iliyopo mkoani Morogoro ili iingie katika mirathi.

Upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Agness Mtunguja aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshitakiwa na jamii inayomzunguka.

Mshitakiwa huyo alifanikiwa kulipa faini hiyo na kuepuka kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Katika kesi hiyo ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2020 na Juni 2020 maeneo tofauti katika mkoa wa Dar es salaam mshitakiwa aliiba Sh 198,750,000 kutoka katika akaunti ya marehemu mume wake.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *