Aliyekufa ajali ya mti Bukoba kuzikwa leo jioni
KIJANA mkazi wa kata ya Rwamishenye Manispaa ya Bukoba aliyefariki Baada ya kuangukiwa na mti kutokana na mvua yenye upepo mkali iliyonyesha alfajiri ya Oktoba 18, 2023 anatarajiwa kuzikwa leo jioni kijijini kwao Bwanjai Wilaya ya Missenyi Mkoa wa Kagera.
Kwa mujibu wa diwani wa kata ya hiyo, Sued Kagasheki amesema kabla ya mvua kunyesha kijana huyo alikuwa akienda katika majukumu yake ya kazi na alipeperushwa na upepo na kuangukiwa na mti na kufariki papohapo.
Alisema kuwa katika kata yake mtaa wa ‘National Housing’ ndio ulioathirika zaidi huku baadhi ya nyumba zikiezuliwa na miti kuanguka.
Kufuatia mvua hiyo Hospitali ya Rufaaa ya Mkoa Bukoba ilipokea majeruhi watatu na kwa mujibu wa Dk Museleta Nyakiroto Mganga mfawadhi wa hospitali hiyo alisema kati ya majeruhi watatu walipokelewa Jana wawili wanaendelea vizuri, mmoja atapata rufaaa kwenda Bugando kwa uchunguzi.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia maswala ya Afrika Mashariki akifanya mahojiano kwa njia ya simu alisema kuwa ofisi ya mbunge kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya imefanya tathimini na kubaini kuwa kaya 241 sawa na watu 1,200 wamepoteza makazi yao.
Alisema ofisi yake inaendelea kubaini mahitaji ya Wananchi hao ili kutoa msaada ingawa wengi wamekiri kupoteza chakula na magodoro kuharibika pamoja na nguo zao hivyo mbunge huyo anajiandaa kujua aanze kushughulikia kitu gani wakati serikali nayo ikijipanga kuhudumia.
“Niko Arusha katika majukumu lakini ni kweli baada ya tathimini na kujua nahitaji ya Wananchi nitajua cha kufanya zaidi, lakini nimewasiliana na ofisi ya Waziri Mkuu juu ya hayo maafa nao wamepiga wilayani hivyo serikali nayo inashughulikia ,niwaombe Wananchi wawe wavumilivu na waendelee kuchukua tahadhari niko pamoja nao.”alisema Byabato.
Mbunge wa Viti maalumu, Neema Rugangira ametoa msaada wa blanketi 50 na magodoro 20 kwa ajili ya wahanga msaada huo umekabidhiwa na katibu wake Mansoor Amri kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima.