Aliyekutwa na viungo vya siri afutiwa kesi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemfutia kesi mkazi wa Simiyu, Salum Nkonja ya kukutwa na viungo vya siri vya binadamu na vya wanyama na imeamuru asikamatwe hadi ushahidi wa shauri lake utakapokamilika.
Pia mahakama imeagiza vielelezo vilivyowasilishwa awali ambavyo ni viungo vya siri vya binadamu viteketezwe.
Hayo yalijiri mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalila kesi hiyo ilipopelekwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ushahidi.
Hakimu Rugemalila alisema uamuzi huo umetokana na mazingira ya mwenendo wa kesi hiyo, kwa upande wa mashtaka kushindwa kukamilisha vielelezo na kuomba ahirisho mara kwa mara na pia kesi hiyo iliwahi kufutwa na kufunguliwa upya mara mbili.
Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwaka 2017 kwa mashtaka ya mauaji, baadaye mwaka 2020 alifutiwa kesi hiyo na kufunguliwa upya kesi ya uhujumu uchumi lakini nayo ilifutwa Juni, 2022 na kufunguliwa tena ikiwa na mashtaka yale yale ya mwaka 2020.
“Tangu ifunguliwe upya, kesi hii imekuwa ikiahirishwa kwa madai kuwa mashahidi hawapo au vielelezo havijakamilika, imehirishwa mara tano. Waraka wa DPP umeweka wazi kuwa mtu asifikishwe mahakamani bila upelelezi kukamilika,” alisema.
“Mahakama inaelewa wazi kuwa haiwezi kulazimisha upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi lakini kutokana na mazingira ya shauri hili mshtakiwa alishaachiwa na kushtakiwa mara mbili, kesi hii naifuta na mahakama inaamuru mshtakiwa asikamatwe hadi watakapokamilisha ushahidi,” aliongeza.
Kabla ya kuanza kusikilizwa ushahidi, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliieleza mahakama kuwa shahidi aliyepaswa kutoa ushahidi alikuwepo lakini vielelezo vilikuwa havijakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kusikilizwa.
Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa utetezi, Mohamed Majaliwa ambaye alidai kuwa kesi hiyo imekuwa ni ya muda mrefu, upande wa mashtaka ukishindwa kukamilisha vielelezo hivyo na aliomba mahakama itoe amri ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Mwanga alidai ikiwa kesi hiyo itaendelea kusikilizwa siku hiyo, ushahidi utasikilizwa nusu kwa kuwa itawalazimu wawasilishe vielelezo siku nyingine jambo ambalo Hakimu Rugemalila hakukubaliana nalo na kuamua kuifuta.
Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 11 na kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ilidaiwa kuwa katika shitaka la kwanza hadi la nane, kati ya Oktoba 30 na Novemba 30, 2017 katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alikutwa akimiliki nyara za serikali zenye thamani ya Sh 20,536,555.
Alidai nyara hizo zilikuwa ni sikio na pembe ya nyati, viungo vitano vya siri vya nyati dume, viungo viwili vya siri vya mbwa mwitu dume, kiungo cha siri cha nyumbu dume, mikia mitano ya ngiri, kiungo kimoja cha siri cha fisi dume, yai la mbuni, ngozi ya ngekewa na kichwa cha nyoka aina ya kobra.
Aliendelea kudai katika shtaka la tisa hadi la 11 kati ya Oktoba 30 hadi Novemba 30, 2017 mshtakiwa huyo alikutwa na viungo vya binadamu ambavyo ni viungo vya siri vya mwanamke na mafuvu mawili.