Aliyemuua mdai wake ahukumiwa kunyongwa

Aliyemuua mdai wake ahukumiwa kunyongwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kunyongwa hadi kufa mshitakiwa Hemed Ally baada ya kupatikana na hatia ya kumuua, Farhani Maluni.

Ally alitenda kosa hilo eneo la Sharifu Shamba Ilala, Dar es Salaam na kumzika mbele ya nyumba aliyokuwa amepanga.

Akisoma hukumu hiyo kwa saa mbili, Hakimu Mkazi Mkuu, Joyce Minde, alisema upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani hapo mashahidi 12 na vielelezo ikiwamo hati ya amri ya kufukuliwa kwa mwili wa marehemu.

Advertisement

Alisema baada ya kupitia ushahidi wote, ameridhika kwamba mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi.

Alisema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulikuwa wa  kimazingira, lakini umeweza kuthibitisha kwamba Ally alikuwa na nia ya kuua kutokana na kushindwa kununua gari aina ya Fusso, licha ya marehemu kumpatia Sh milioni 30.

Hakimu Minde alisema ni lazima mahakama ijiridhishe kwa asilimia 100 endapo kuna ushahidi wa mazingira bila kuacha shaka yoyote kwamba kilichotokea ndiyo uhalisia, hivyo mahakama imejiridhisha kuwa mshitakiwa alikuwa ana nia ovu.

“Upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kuwa kitu kilichofukuliwa Februari 9, 2015 eneo la Sharifu Shamba Ilala, Dar es Salaam kilikuwa ni mabaki ya mwili wa binadamu pia waliweza kuthibitisha kupitia daktari bingwa wa magonjwa ya binadamu na vifo vya mashaka, Innocent Mosha, aliyeeleza kwamba marehemu Maluni kabla ya kuuawa na kufukiwa, alifungwa kamba ya katani mikononi na kichwani pamoja na plasta,” alisema Hakimu Minde.

Hakimu Minde alisema uthibitisho wa masalia ya marehemu yalithibitishwa kutokana na nguo za marehemu zilizopatikana kwenye mabaki hayo ambazo zilithibitishwa na mke wa marehemu, Tatu Ally ambaye alidai ndiyo nguo alizomuandalia mumewe asubuhi.

Akichambua utetezi wa mshitakiwa, Hakimu Minde alisema mshitakiwa hakuweza kuleta ushahidi mahakamani kama alihama kwenye nyumba aliyopanga Sharifu Shamba kwa sababu ya maji na umeme kuunganishwa kinyume cha sheria.

“Upande wa utetezi ulishindwa kuhoji masuala ya msingi na pia kushindwa kuleta vitu vya msingi kuonesha au kuthibitisha alichokidai mshitakiwa kama suala la maji na umeme,” alisema.

Minde alisema mshitakiwa katika utetezi wake, alidai mateso na vipigo ndiyo vilimfanya asaini maelezo ambayo hakuyasema yeye. Alisema lakini mahakama ilijiuliza kama maneno ya maelezo ya onyo na aliyoyatoa mahakamani yanafanana.

“Mahakama iliona maneno yanafanana kwa sababu alichokuwa akiulizwa mahakamani ndicho kilichokuwepo kwenye maelezo ya onyo ikiwemo idadi ya ndugu zake na jina la baba yake mzazi,” alisema.

Baada ya kuelezwa hivyo, Hakimu Minde huku akiwa amesimama alimueleza mshitakiwa kuwa adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Ally alikubaliana na Farhani (marehemu) kumnunulia gari aina ya Fusso na alikabidhiwa Sh milioni 30 lakini alishindwa kumkabidhi gari na alipanga njama za kuua.

Maelezo ya hati hiyo ya mashitaka yanasema Ally alimuua Farhan, Juni 12, 2014 maeneo ya Sharifu Shamba Ilala, jijini Dar es Salaam kisha akauzika mwili wake nje karibu na mlango wa kuingilia katika nyumba aliyokuwa akiishi.

Hata hivyo, mwili huo ulifukuliwa na Jeshi la Polisi Februari 9, 2015, takribani miezi minane baadaye kwa ajili ya uchunguzi, baada ya polisi kupata taarifa kuwa mshitakiwa alimuua na kuuzika mwili huo mahali hapo.

 

/* */