Aliyeshinda kesi ya mashamba auawa kwa kukatwa mapanga

MKAZI wa Kijiji cha Malulu, Kata ya Didia Halmashauri ya Shinyanga, Shoma Moshi (50) ameuawa na watu wasiojulikana kwa kukatwa mapanga wakati akimuogesha mjukuu wake majira ya saa mbili usiku nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alithibitisha tukio hilo lililotokea tarehe 30/10/2022 katika Kijiji cha Malulu, Kata ya Didia.

Kamanda Magomi alisema chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa kuwa ni ugomvi wa mashamba baada ya mwanamke huyo kushinda kesi mahakamani na kukabidhiwa mashamba yake.

Advertisement

Kufuatia matukio ya watu kujichukulia sheria mkononi, Kamanda Magomi amewataka wananchi kufuata sheria badala ya kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia ambayo yangemalizwa kwa kushirikisha vyombo husika.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Malulu, Senga Shimba alisema tukio la mauaji limeshtua wananchi na ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliomuua mama huyo kwa kumkata mapanga.

Shimba alisema mama huyo alishinda kesi ya ardhi kwenye mahakama ya baraza la ardhi na aliyekuwa na mgogoro naye ametoweka baada ya mauaji kutokea.

Mtoto wa marehemu, James Joseph alisema kifo cha mama yake kimemsikitisha kutokana na kuuawa kikatili kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Naye ameiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kuwabaini waliohusika na kuwachukulia hatua kali.