Aliyetuhumiwa kunajisi mtoto wa miaka 5 ashinda rufani

MAHAKAMA Kuu Masjala ya Wilaya ya Mwanza, imemwachilia huru Daudi Kanyengele baada ya kushinda rufaa aliyofungua kupinga kifungo cha miaka 30 jela, aliyohukumiwa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumnajisi binti wa miaka 5.

Hukumu hiyo iliyochapwa katika tovuti ya mahakama ilitolewa Juni 23, 2023 na Jaji Mwanabaraka Mnyukwa ambaye alisema uamuzi huo ulitokana na ushahidi uliotolewa wakati wa kusikilizwa shauri katika mahakama ya chini.

Katika rufani hiyo, Kanyengele alisimamia katika hoja kadhaa ikiwemo kwamba mahakama ya chini ilikosea kisheria kumtia hatiani kwa kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote wa kitabibu kwamba binti huyo aliingiliwa, kwamba mahakama ya chini ilikosea kumtia hatiani kwa kuwa mwathirika hakueleza kwa kina aina ya mwanga uliokuwepo kumwezesha kumtambua kwa kuzingatia kuwa tukio lilitokea usiku.

Advertisement

Pia alidai kwamba mahakama ilikosea kumtia hatiani kwa ushahidi wa binti huyo ambao haukuwa umethibitishwa na kwamba umri wa mtoto haukuthibitishwa badala yake mahakama iliangalia tu maumbile ya mtoto wakati kuna watu huwa wamethiriwa na umbilikimo.

Katika uamuzi wake Jaji Mnyukwa alisema msingi wa rufaa ni kwamba mrufani anasimamia hoja kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka na kumekuwa na ukiukwaji wakati wa kuendeshwa shauri hilo katika Mahakama ya chini.

Alisema kwa ujumla ushahidi wa mwathirika hakuwa wa nguvu ya kutumika kumtia hatiani mrufani isipokuwa kama ungeambatanishwa na vielelezo vingine na si kwa maelezo matupu na aliongeza kuwa ili mahakama iweze kupata ushahidi mzuri ni lazima shahidi awe wa kuaminika na lazima kuwe na uwiano wa ushahidi mwathirika na mashahidi wengine.

“Katika kesi hii mahakama iliegemea zaidi katika ushahidi wa mwathirika na hata hivyo hakukuwa na uwiano kwa kuwa mwathirika alisema baada ya tukio alikwenda nyumbani na kuwakuta ndugu zake akiwemo dada yake Jenifer lakini kwa upande wa Jenifer alidai kuwa yeye ndiye alimfata mdogo wake kwa jirani na baada ya kufika nyumbani ndiyo mdogo wake alimweleza kuwa mrufani alimbaka,” alisema Jaji Mnyukwa.

“Kwa kuzingatia yote yaliyojadiliwa wakati wa kusikiliza shauri, mahakama inapuuzia ushahidi wa mwathirika kwa kuwa unashindwa kuthibitisha mashtaka katika viwango vinavyotakiwa, inawezekana ni kweli mwathirika alibakwa lakini upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kwamba alikuwa ni mrufani ndiye aliyembaka,” alisema.

“Kama ilivyoelezwa kuwa si kazi ya mrufani kuthibitisha kutokuwa na hatia kwake wakati anapoonesha shaka katika uamuzi wa mashtaa dhidi yake, na katika utetezi wake alieleza kutotenda kosa hilo na alikana kumfahamu mtoto huyo,” alisema.

Kwa kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka umeshindwa kumtambua mrufani ni wazi kuwa walishindwa kuthibitisha mashtaka kwa viwango vinavyopaswa, hivyo naruhusu rufani kwa sababu utambulisho wa mrufani na sifa za binti vilitia shaka, kwa maana hiyo namuondolea mrufani hatia na kumuondolea kifungo, mrufani anapaswa kuachiwa huru isipokuwa kama zipo sababu nyingine za kisheria za kumshikilia.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *