Aliyeuwa kisa pesa ya umeme akamatwa Arusha

JESHI la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwanamke mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Blandina Fred ,26 mkazi wa kijiji cha Elkilevi kata ya Oltoroto wilayani Arumeru kwa tuhuma ya kuua kwa kutumia kisu.

Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Justin Masejo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano.

Masejo alisema kuwa polisi inafanya mahojiano na mtuhumiwa na uchunguzi mwingine unafanyika kwa mujibu wa taratibu na uchunguzi ukikamilika jalada litafikishwa kwa mwanasheria wa serikali kwa taratibui zingine kufanyika.

‘’Kweli tukio lipo na mtuhumiwa tunamshikilia kwa ajili ya mahojiano na taratibu zingine’’ alisema Masejo

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Elikilevi, Abrahamu Mollel ilidaiwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya kati ya saa 5 na saa 7 mchana katika Kijiji hicho lilisababishwa na ugomvi wa fedha za malipo ya luku kwa ajili ya nyumba wanayopanga.

Mollel alisema kuwa mtuhumiwa Blandina Fred alibishana na marehemu Erick Adamu ,32, ambaye inadaiwa kuwa ni msanii wa muziki wa bongo fleva juu ya malipo ya luku ya kati ya Sh 1,000 hadi 2,000 kwani siku hiyo ilikuwa zamu yake.

Alisema katika madai ya malipo hayo ilielezwa kuwa msanii huyo alibisha kwani hakuwa na uhakika kama yeye ilikuwa zamu yake na kuzuka ubishi uliopelekea Blandina Fred kuchukua uamuzi wa kumchoma kisu shingoni  kufa hapo hapo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa mwili wa msanii huyo uko katika Hospital ya Rufaa ya Mount Meru na amewataka wapangaji wa nyumba hiyo kuwa na uvumilivu kusubiri taratibu za kipolissi.

Mpangaji katika nyumba hiyo ambaye aliomba kuhifadhiwa jina alisema kuwa msanii huyo hakuwa mbishi katika malipo ya Sh  1,000 hadi 2,000 ya luku kwani lugha ya kashfa na ubabe ndio ilimkasirisha na kuamua kugoma kulipa ndipo uamuzi wa kuchomwa kisu ulipozuka.

‘’Ni lugha za kudhalilishana na ubabe zilizuka kwa wawili hao ndio zilizozua kifo kwa msanii huyo ‘’alisema mpangaji huyo

Habari Zifananazo

Back to top button