Amani, utulivu vyatawala Krismasi

WAKATI juzi Watanzania wakisheherekea Sikukuu ya Krismasi, Jeshi la Polisi katika mikoa mbalimbali limesema hali ilikuwa shwari na kuwepo kwa matukio machache ya uhalifu.

Matukio machache ya kihalifu yaliyotokea yametajwa ni wizi wa simu, ugomvi mdogomdogo na ajali ndogo za bodaboda. Kamada wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alisema jana kuwa mkoa huo upo shwari na wananchi wake wamesherehekea Sikukuu ya Krismasi kwa amani na utulivu.

“Siku za sikukuu ya Krismas, kuanzia mkesha na siku ya sikukuu yenyewe, kwa Dodoma hali ni shwari, hatuna matukio makubwa zaidi ya ugomvi mdogomdogo wa mtu kagombana na mwenzake na ambayo ni matukio kidogo sana,” alisema.

Kwa upande wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema hali ya usalama katika sikukuu hiyo ilikuwa shwari, hakuna matukio makubwa ya kiuhalifu yaliyojitokeza.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema jeshi hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na kuzuia uwepo kwa matukio ambayo yangeweza kujenga hofu au madhara kwa jamii.

“Kwa ujumla hali ya kiusalama jana (juzi) ilikuwa ni nzuri na hakukuwa na matukio yoyote makubwa ambayo yangeweza kujenga hofu au ambayo yameweza kuleta athari yoyote kwenye jamii lakini kuliwepo na matukio madogomadogo kama watu kuibiwa simu, ugomvi mdogomdogo na bodaboda kugongana bila kupata madhara makubwa mwilini,’’ alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi alisema hali imeendelea kuwa shwari kwenye nyumba za ibada na hakukuwa na disko toto baada ya kupigwa marufuku.

“Mpaka sasa hali imeendelea vizuri kwa wananchi kusherehekea Sikukuu ya Krismasi. Hatujapokea tukio lolote la uhalifu wala ukatili,” alisema alipozungumza na gazeti hili jana mchana.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema kwenye sikukuu, jeshi hilo lilifanya doria maeneo mbalimbali ya mikusanyiko na hakukuwa na matukio ya uvunjifu wa amani.

Kamanda Kuzaga aliwataka wananchi mkoani humo kuelekea Sikukuu ya Mwaka Mpya kutozidisha furaha ambayo itawafanya kutenda uhalifu hususani madereva wa vyombo vya moto na wale wanaokwenda kusheherekea kwenye kumbi za starehe kuhakikisha wanakuwa watulivu na kufuata taratibu zilizowekwa na nchi. Aliwataka wananchi kutoacha kaya zao bila uangalizi ili kuzuia uhalifu unaoweza kujitokeza pindi wanapokuwa katika maeneo ya sherehe.

Aliongeza kuwa kutokana na utaratibu ambao Jeshi la Polisi limeuandaa wa kupima kiwango cha ulevi kwa madereva wote mkoani humo, imesaidia kupunguza ajali zilizokuwa zikitokea kwa wingi kipindi cha sikukuu.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Ally Kitumbu alisema Jeshi la Polisi limefanya msako na kudhibiti uuzaji holela wa pombe ya gongo kipindi hiki cha Sikukuu Krismasi.

Alisema msako umefanyika na baadhi ya wahusika wamekamatwa na kudhibitiwa kwani pombe hiyo imekuwa chanzo cha matukio ya kihalifu.

“Sisi tumejipanga na tunaendelea vizuri, vilevile msako umefanyika na tunaendelea kukusanya taarifa mbalimbali, ili tuhakikishe kwamba Krismasi tunaimaliza salama na mwaka mpya tunafika salama,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale, aliliambia HabariLEO kwamba hali ya usalama mkoani kwake iko shwari, hakuna matukio yaliyoripotiwa juzi na jana.

Alisema jeshi linaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote ikiwemo sehemu za fukwe na barabarani. Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu alisema jana mjini Morogoro kuwa jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha linadhibiti vitendo vya uhalifu hasa kipindi hiki cha kuelekea mwaka mpya 2023.

“Tunaumaliza vizuri mwaka 2022 na tunauanza vyema mwaka 2023. Tunahakikisha watu wanakuwa salama na mali zao,” alisema.

Habari hii imeandikwa na Anastazia Anyimike (Dodoma), Rehema Lugono (Dar), Kareny Masasy (Kahama), Shukuru Mgoba (Mbeya), Yohana Shida (Geita), Abela Msikula (Kagera) na John Nditi (Morogoro).

Habari Zifananazo

Back to top button