Anayedaiwa kujifanya Rais Samia akana vielelezo kortini

Mahakama yaahirisha uchunguzi kifo cha mahabusi

MSHITAKIWA Nickson Mfoi (20) aliyetumia jina la Rais Samia Suluhu Hassan kutapeli ameikana laini ya simu na vielelezo vingine vilivyofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anavyodaiwa kuwa alikuwa akivitumia kwenye utapeli.

Mfoi anakabiliwa na mashitaka ya kujitambulisha mtandaoni kama Rais Samia na kutumia laini ya simu iliyo katika umiliki wa mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

Mfoi amevikana vielelezo hivyo juzi mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

Advertisement

Vielelezo hivyo ni hati ya ukamataji mali, hati ya uchunguzi wa simu, simu aina ya Infinix Hot10i, laini ya simu ya mtandao wa Airtel, fomu ya usajili wa mtandao, maelezo ya onyo pamoja na fomu ya mnyororo wa utunzaji vidhibiti.

Akiongozwa na wakili wa serikali, Ashura Nzava, Mfoi alidai kuwa awali alikubali kuwa alichukuliwa simu iliyotajwa katika maelezo kwa kuwa ilihusishwa na eneo ambalo alikamatiwa. Pia simu yake haikuwa Infinix Hot10i ambayo imeletwa mbele ya mahakama isipokuwa simu yake ilikuwa ni Infinix Mark X.

Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Septemba 22 mwaka 2021 nchini kwa nia ya ulaghai na udanganyifu, Mfoi alijitambulisha mtandaoni kama Rais Samia jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Katika mashtaka ya pili mshtakiwa alikutwa akimiliki na kutumia laini ya simu iliyo katika umiliki wa mtu mwingine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

Katika mashtaka hayo, ilidaiwa Oktoba 2, 2022 hapa nchini, mshtakiwa huyo alikutwa akitumia laini hiyo yenye namba 0686 623299 iliyo katika umiliki wa jina la Getness Jackson bila kutoa taarifa ya mabadiliko ya umiliki kwa mtoa huduma.

Mshitakiwa amerudishwa rumande hadi Oktoba 18 mwaka huu.