Anayedaiwa kuua mke aomba aachiwe huru

MSHITAKIWA Khamis Luwonga, anayekabiliwa na mashitaka ya kumuua mkewe Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, ameiomba Mahakama Kuu imuachie huru kwa sababu hadi sasa hakuna ushahidi wa kutosha kumshitaki.

Luwonga aliwasilisha ombi hilo leo mbele ya Jaji, Obadia Bwegoge kupitia kwa Wakili wake, Mohamed Majaliwa na kuiomba mahakama kesi ya mauji namba 5, ya mwaka 2022 iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa ina mapungufu ya kisheria.

Advertisement

Majaliwa alidai kuwa mteja wake anashitakiwa kwa kosa la mauji mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rhoda Ngimilanga wa Mahakama ya Kisutu, alidai shauri hilo linaonekana jipya lakini kiuhalisia sio jipya kwa sababu kesi ya mauji namba 4, ya Mwaka 2019 dhidi ya mshitakiwa ilishaisha. 

Alidai kuwa mashitaka yaliyokuwepo kwenye hati hiyo yalipita katika hatua zote za kisheria na Oktoba 24, mwaka 2022 kesi iliitwa kwa ajili ya kusikilizwa ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne. 

Majaliwa alidai kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwasiti Ally alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga wa Mahakama ya Kisutu kuwa kesi ililetwa kwa ajili kusikilizwa, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mshitakiwa. 

Alidai kuwa kutokana na kuomba kuondolewa kwa kesi hiyo, Hakimu Ruboroga alimuachia Luwonga, lakini cha kushangaza mshitakiwa alikamatwa tena na askari na baada ya saa chache alipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashitaka yale yale. 

“Hadi sasa hivi jalada lililokuwa mbele yako linaonesha upelelezi bado haujakamilika ni rai yetu kwamba mashitaka haya mapya ni batili mbele yako kwa sababu yanakiuka sheria,” alidai Majaliwa 

Majaliwa alidai sheria imetoa utaratibu kama mtu akiachiwa na serikali ikataka kumshitaki tena basi ni lazima kuwepo na ushahidi wa kutosha na usikilizwaji wake uanze mara moja, lakini katika kesi hiyo hilo halikuzingatiwa. 

Ukijibu hoja hizo, upande wa mashitaka ulidai kuwa mahakama hiyo imefungwa mikono kutoa amri kwenye amri ambazo hazijafika mwisho na pia uhalisia wa mashitaka ya mauaji ni lazima mshitakiwa awe commited 

Katika hoja ya kuachiwa kwa mshitakiwa, upande huo ulidai kuwa hoja hiyo inakinzana na matakwa ya kisheria na pia taratibu za kisheria bado hazijakamilika, kwa sababu kesi bado haijafika Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa. 

Baada ya Jaji Bwegoge kusikiliza hoja za pande zote mbili, aliahirisha maombi hayo hadi Aprili 18, mwaka huu kwa ajili ya uamuzi.

Luwonga amefungua maombi Mahakama Kuu ili wampatie maelezo ya uhalali wa kesi namba 5, ya Mwaka 2022 ya mauji baada ya kesi ya awali ya mshitakiwa huyo kufutwa na kufunguliwa upya. 

Katika kesi hiyo ya muaji namba nne ya mwaka 2019, mshitakiwa Luwonga ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni alimuua Naomi Marijani.

Khamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake.

/* */