Anayedaiwa kuua mke asomewa mashitaka mapya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imempandisha kizimbani na kumsomea upya mashitaka ya mauaji mfanyabiashara Khamis Luwonga.

Awali, mashitaka hayo yalifutwa kwa kile kilichoelezwa mahakamani hapo kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliondoa nia ya kuendelea na shauri hilo.

Hayo yalijiri Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga. Upande wa mashitaka uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Mwasiti Athumani.

Akisoma mashitaka mapya, Mwasiti alidai Mei 15, 2019, Gezaulole, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Luwonga alimuua Naomi Marijani ambaye alikuwa mke wake.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Luboroga, Wakili Mwasiti alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya kusikiliza ushahidi, lakini DPP alionesha nia ya kutoendelea na shauri hilo.

“Mheshimiwa shauri hili lilikuja kwa ajili ya kutajwa, upande wa mashtaka tulikuwa nao mashahidi wanne, lakini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mshitakiwa, hii ni chini ya kifungu cha 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,” alisema Wakili Mwasiti.

Baada ya kusikiliza hoja hiyo, Hakimu Luboroga alimuachia huru mshitakiwa.

Hata hivyo, kabla ya kutoka mahakamani mshitakiwa aliomba ruhusa ya mahakama azungumze.

Katika sehemu ya maelezo yake, mshitakiwa huyo alidai ana maumivu makali ndani ya moyo wake kwa tukio analoshitakiwa nalo huku baadhi ya Watanzania wakiwa na mioyo ya dharau kwa kushindwa kuzuia matatizo kabla jambo la hatari halijatokea.

Alidai watu siku zote huwa wanapenda kuangalia uharibifu uliotokea, lakini hawaangalii mwanzo wa uharibifu na kudai kuwa yeye si chanzo cha kifo cha mkewe, bali ndugu wa pande zote.

Alidai kuwa mkewe alikuwa akitaka kifo hicho kwa kukiomba kwa Mungu kila kukicha na kusababisha mtoto wao wa pekee aishi maisha ya upweke, bila wazazi.

“Vitabu vya dini vinasema unapomuona mtu amekengeuka, mrekebishe awe katika njia sahihi, mke wangu mpenzi nitaendelea kusimamia ukweli kwamba ndugu upande wangu, upande wa mke wangu, viongozi wa Serikali wa Mtaa, Polisi wote walisababisha kifo cha mke wangu,” alidai Luwonga.

Alisema ndugu wa mkewe wamesababisha mtoto wake anaishi maisha magumu na hana uhakika kama analipiwa ada huku lawama kuwa ndugu wa mke wake wamezuia ndugu zake wasimuone mtoto wake jambo ambalo anasema linaweza kuleta shida baadaye.

Baada ya kusikiliza hoja zake, Hakimu Luboroga alimweleza mshitakiwa kwamba suala la mtoto ni mambo ya familia hivyo ndugu wa pande zote wanapaswa kukaa chini na kutafuta suluhu kwani tayari kesi hiyo ilishaondolewa mahakamani

Habari Zifananazo

Back to top button