Andengenye aahidi Neema kwa Machinga

KIGOMA: Serikali mkoani Kigoma imeahidi kuendelea kuunga mkono maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwa serikali za mikoa na wilaya kushirikiana na wafanyabiashara wadogo maarufu machinga kwa kuwatengea maeneo ambayo yataruhusu kufanya biashara zao kwa tija.

Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye amesema hayo alipokutana na viongozi wa shirikisho la machinga Mkoa wa Kigoma (SHIUMA) ili kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na namna ambavyo changamoto hizo zinaweza kutatuliwa kwa pamoja baina ya wafanyabiashara hao na serikali.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa kundi hilo kwa kuwa linayagusa maisha ya watu wengi  na kwamba uongozi serikali  mkoani humo  utaendelea kutafuta na kutenga  maeneo mapya ambayo yataruhusu wajasiriamali kufanya biashara kwa tija huku suala la usalama wa afya na biashara zao likizingatiwa.

Advertisement

Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa SHIUMA Mkoa wa Kigoma, Ali Mvano amesema  kuwa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maeneo yanayoruhusu biashara zao kufanyika kwa tija lakini pia changamoto ya mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha na taasisi za maendeleo ikiwemo fedha kutoka kwenye halmashauri.

Aidha Mvano alisema kuwa bado hakuna takwimu kamili za idadi ya wafanyabiashara hao wadogo na kupitia kikao hicho alitoa wito kwa wajasiriamali wanaofanya shughuli zao nje ya shirikisho kujiunga ili kupata haki zao pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *