Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ameitaka sekta ya mahakama kusimamia haki kwa uwazi ili haki hiyo ionekane imetendeka kuwezesha kuchochea ustawi katika jamii na kuleta maendeleo ya nchi.
Andengenye amesema hayo akizindua wiki ya sheria ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi kwa kushughuli za mahakama uzinduzi uliofanyika kwenye viwanja vya Mwanga Centre mjini Kigoma.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa maendeleo kwa kiasi kikubwa yanategemea kuwepo kwa utendaji haki na mahakama ndiyo chombo kilichopewa mamlaka na madaraka ya kusimamia jambo hilo.
Huku akinukuu vitabu vya dini vinavyoeleza kuwa haki huinua taifa na kwamba bila haki hakuna maendeleo katika taifa lolote mkuu huyo wa Mkoa Kigoma alisema kuwa Mkoa Kigoma unapiga hatua za maendeleo kwa haraka na kwa sasa serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza miradi mkoani humo hivyo ni lazima suala la utendaji haki liwe linaonekana wazi katika utendaji wa idara ya mahakama.
Awali Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma, Augustine Rwizile amesema kuwa matumizi ya mfumo wa mahakama mtandao (TEHAMA) katika kushughulikia mashauri umewezesha kuwepo na uwazi na uwajibikaji katika usikilizaji wa mashauri.
Jaji Rwizile alisema kuwa kuwa mahakama mtandao imewezesha kuonyesha mwenendo mzima wa kesi tangu inasajiliwa hadi kusikilizwa jambo linalotoa nafasi kwa wadau wote wa haki jinai kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mashauri kwenye idara ya mahakama kwa ngazi zote.