ANTU: ‘Uwekezaji Bandari Dar utawainua wamachinga’
DAR ES SALAAM: UWEKEZAJI katika Bandari ya Dar es Salaam umeelezwa kuwa ni chachu ya mafanikio kwa wafanyabiashara ndogo ndogo ‘wamachinga’ hapa nchini.
Akizungumza katika kongamano la wamachinga wa wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam leo, Jumamosi katika viwanja vya Biafra, Mkurugenzi wa Shirika la Vijana Imara (VIO), Antu Mandoza amesema uwekezaji wa bandari hiyo utasaidia bidhaa kuondolewa mapema mara zingiapo kutoka nje ya nchi, jambo litakalosaidia kupungua kwa gharama.
Katika kongamano hilo lililotanguliwa na maandamano ya wafanyabiashara hao, Antu ameelezea matumaini yake ya kufunguka kwa biashara maeneo mbalimbali ya nchi baada ya Serikali kuingia makubaliano na Kampuni ya DP World katika uendeshaji wa baadhi ya maeneo katika bandari hiyo.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo ametoa rai kwa Serikali kuhakikisha kuwa wamachinga hawabughudhi wakati wanatekeleza majukumu yao ya kujitafutia kipato huku ashauri kurasimishwa baadhi ya maeneo kurahisisha bishara za usiku.
“Wamachinga wasibughudhiwe, turasimishe magulio ya usiku kwani biashara zinakwenda kufunguka,” amesisitiza huku akishangiliwa na wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, amewataka wamachinga kutumia simu janja kuweza kuwafikia wateja hadi nyumbani na kwa bei nafuu kwani ulimwengu unabadilika kwa kasi, jambo linalosukuma mabadiliko katika nyanja mbalimbali.
Akimwakilisha mwenyekiti wa umoja wa machinga taifa, Ernest Matondo, Makamu Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Steven Lusinde ameshauri wafanyabiashara wadogo waondolewe masharti magumu ili waweze kufanya biashara katika maeneo ya kisasa ambayo yanatengenezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Alimgeukia Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saadi Mtambule, na kumwagia sifa kwa ujenzi wa soko la kisasa katika eneo la Mwenge lakini wengi wa wanachama wanashindwa kutumia fursa hizo kutokana na masharti aliyodai yanawakwamisha.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni alikiri kuwa Serikali imeona mchango mkubwa wa kundi hilo, ndiyo maana imeandaa mpango kabambe utakaowawezesha wamachinga kumiliki ardhi kwa ajili ya makazi.
Kwa mujibu wa DC Mtambule, wanachinga wanaweza kutumia rasilimali hiyo na kuweza kukopesheka zaidi.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kwa sasa serikali inawaunganisha wamachinga na taasisi za kifedha ili waweze kukopeshwa hadi Shilingi Milioni mbili bila riba.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Hatua kwa Hatua na Mama, Amur Mussa amesema taasisi hiyo imeanzishwa mahususi kwa lengo la kuunga mkono jitahada za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye serikali yake imekuwa ikibuni namna ya kuliinua kundi hilo hapa nchini.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Nandera Mhando amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa kanzidata ya kitaifa kwa lengo la kuwaunganisha wafanyabiashara ndogo ndogo na kuwatambua ili kurasimisha waweze kupata mikopo na huduma nyingine za kijamii.
Naye Mohamed Athuman Ali, Mkuu wa Idara ya Habari ya Machinga akisoma risala ametoa ombi kwa Serikali kuwafadhili wamachinga ili waweza kuingia katika mpango wa bima ili waweze kupata huduma ya afya bila kutaabika.