UJIJI, Kigoma: MPANGO wa uanzishwaji wa anuani za makazi umekuwa kichocheo kikubwa katika utekelezaji wa shughuli za serikali ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama na mipango ya serikali katika utekelezaji miradi ya uchumi kwa wananchi.
Mkurugenzi wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Mwantumu Mgonja amesema hayo akielezea mpango unaoendelea nchini, chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kufanya maboresho ya zoezi la anuani za makazi kwa kuhuisha taarifa na miundombinu iliyofanyika kwa kipindi kilichopita sambamba na kuhuisha na kukusanya taarifa mpya.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika upangaji na utekelezaji wa shughuli zake za kiuchumi anuani zilizopo kwenye taarifa za watu mbalimbali wanaofanya nao shughuli mbalimbali za kiuchumi wamekuwa wakifikika kwa urahisi na kwa usahihi bila kupoteza mud ana hivyo imesaidia kuifanya halmashauri kuwafikia wadau wake mbalimbali ambao wanashirikiana nao kwenye masuala ya uchumi na maendeleo.
Akizungumzia utekelezaji huo, Mtaalamu wa mfumo wa anwani za makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Charles Semzaba amesema kuwa ni muendelezo wa uboreshaji wa taarifa za anuani za makazi kwa kufanya uhakiki na kuingiza taarifa za watu ambao hawakuwemo kwenye mpango huo.
Awamu hii halmashauri 16 zinatekeleza mpango huo wa maboresho ya anuani za makazi ikiwa ni awamu ya kwanza ya mpango huo lengo likiwa kuzifikia halmashauri zote nchini na kwamba taarifa za watu kuhama au kuhamisha shughuli zao zimekuwa zikitokea kila wakati hivyo mpango huo utawezesha kurekebisha taarifa hizo.
Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake kuanza kutekelezwa kwa mpango huo wa maboresho ya anuani za makazi, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Ntime Mwalyambi amesema kuwa maboresho hayo ni muhimu kuweka usahihi wa taarifa ili waliopo kwenye taarifa hizo wawe na uhakika wa kukutwa kwenye maeneo ambayo taarifa zao zinaonyesha.
Mwalyambi amesema ni jambo muhimu kwa serikali katika kupanga shughuli za kiuchumi, Ulinzi, usalama, kuzuia maafa lakini katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambapo taarifa zitabainisha kila mkazi na usahihi wa mahali anapoishi au kufanya shughuli zake.