Aomba EU iwezeshe benki za TADB, TIB kupaisha BBT

RAIS Samia Suluhu Hassan ameuomba Umoja wa Ulaya (EU) uiwezeshe Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) ili ziimarishe mradi wa kuwezesha vijana kulima kibiashara (BBT). Rais Samia alimuomba hayo Balozi wa EU nchini, Manfredo Fanti ambaye anamaliza muda wake.

Pia alitaja maombi mengine kuwa ni kufahamu muundo wa makubaliano ya ushirikiano kati ya EU na umoja wa mataifa ya Afrika, Caribbean and Pacific States (OACPS) na pia kukiingiza kiwanja cha ndege cha Mwanza kwenye miradi ya viwanja vya ndege ili kiboreshwe kiwe cha kimataifa.

Pia alishuhudia Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Natu Mwamba na Balozi huyo wa EU nchini, Fanti wakisaini mikataba mitatu ya kifedha yenye thamani ya Sh bilioni 455, Dodoma jana.

Advertisement

Rais Samia alisema serikali inatarajia kuzitumia TADB na TIC kuwezesha vijana kugharamia BBT hivyo akaomba EU ione namna ya kuziwezesha benki hizo katika mikopo.

Rais Samia alimpongeza Balozi Fanti kwa kufanya kazi nzuri iliyoimarisha ushirikiano wa EU na Tanzania na kuwezesha kiwango cha biashara baina yao kukua kutoka Dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2019 hadi dola za Marekani bilioni 2.1 mwaka jana.

Alisema kuimarika kwa ushirikiano wa EU na Tanzania kumewezesha ongezeko la idadi ya watalii nchini kwa wananchi wa umoja huo 362,393 mwaka 2019 hadi 449, 200 mwaka jana.

Rais Samia alisema kongamano la biashara kati ya EU na Tanzania lililofanyika mwaka huu limetoa fursa kwa jumuiya ya wafanyabiashara nchini kuzitumia fursa kwenye uchumi wa dunia.

“Kabla ilikuwa haiwezekani lakini sasa wanaweza kwenda mbali kadiri wanavyotaka,” alisema na kuongeza kuwa mjadala wa kisiasa baina yao Februari mwaka huu umewezesha nchi kuitumia Ulaya kutatua migogoro na kuzuia ugaidi. Rais Samia pia alimuomba Fanti aendelee kuwa Balozi wa Tanzania na akamuahidi kutekeleza mambo matano aliyomuachia ya kitaifa na kimataifa.