Apongeza mwamko matumizi taarifa hali ya hewa

Dk Agnes Kijazi

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agnes Kijazi  amesema kumekuwa na mwamko mzuri wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu na uelewa kwa wananchi umeongezeka.

Alibainisha hayo Jumatano  Kibaha wakati akifungua warsha ya wanahabari kuhusu utabiri wa msimu wa vuli (Oktoba hadi Desemba, 2022) unaotarajiwa kutolewa kesho.

“Mafunzo haya kwa wanahabari yameleta mwamko na uelewa kwa wananchi na siku hizi wananchi wamekuwa wakipiga kuulizia taarifa za hali hewa kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo… Taarifa zikiwafikia kwa wakati zitawasaidia kujipanga,” alisema.

Advertisement

Alisema taarifa hizo pia ni muhimu kwa mamlaka au sekta zingine kupanga mipango ya maendeleo na kukabiliana na maafa.

Kuhusiana na warsha hiyo ya wanahabari alisema inalenga kutoa taarifa kwa wakati na sahihi na kuwa utabiri umekuwa ukisaidia sekta kama kilimo, nishati, maji na sekta nyingine ambazo zinahitaji taarifa hizo muhimu za hali ya hewa.

Alisema taarifa na ushauri unaotolewa na TMA utasaidia sekta husika kujipanga kwa shughuli za maendeleo na kuleta tija na ndio maana wataalamu wameandaa rasimu na viashiria ili pia jamii ipate uelewa wa utabiri unaotolewa kwa njia za kijadi na kisasa.

Dk Kijazi alisema pia utabiri ukiwafikia wadau kwa wakati utasaidia serikali na taasisi na sekta zake kujipanga kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Aliwataka na kusisitiza wananchi kupata taarifa kwa wakati na sahili kutoka TMA badala ya kutafuta taarifa hizo kwenye intaneti.