APR yatolewa Ligi ya Mabingwa

WAWAKILISHI wa Rwanda katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, APR FC wametolewa baada ya kufungwa jumla ya mabao 3-1 dhidi ya US Monastir katika raundi ya awali ya michuano hiyo.

Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Stade Mustapha Ben Jannet, timu ya Tunisia ilishinda mchezo huo kwa mabao 3-0.

US Monastir walipoteza mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Huye kwa kufungwa bao 1-0, lakini wamefanikiwa kusonga mbele hatua inayofuata ya mashindano hayo kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1.

Shuti la mbali kutoka kwa Haykeul Chickhaoui liligonga mwamba, huku kipa wa APR, Pierre Ishimwe akishindwa kuudaka na Zied Aloui aliuwahi mpira huo na kuwa bao la kuongoza dakika sita tangu kuanza kwa mchezo.

Nafasi ya kwanza kwa APR ilikuja katika dakika ya 18 baada ya Yves Mugunga kuangushwa karibu na eneo muhimu la US Monastir, lakini mpira wa adhabu ulitoka nje.

US Monastir ilipata bao lake la pili katika dakika ya 29 kupitia kwa kiungo wake, Houssem Tka aliyeunganisha vizuri mpira katika nyavu kufuatia krosi kutoka kwa Idriss Mhirsi.

Nafasi zilikuwa chache baada ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza, huku US Monastir ikiwa mbele kwa mabao 2-0 na kuwa juu.

Kipindi cha pili kilishuhudia US Monastir ikiendelea kutawala na walifanikiwa kuongeza bao la tatu katika dakika ya 68 kupitia kwa Youssouf Oumarou akiwa ndani ya boksi.

Beki ya APR waliweza kuwazuia washambuliaji wa US Monastir katika dakika 15 za mwisho za mchezo huo wakati mwamuzi akipuliza filimbi ya mwisho kumaliza mchezo huo.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button