Arusha yang’ara miradi ya uwekezaji
MKOA wa Arusha umeongoza kwa kufungua miradi 13 ya uwekezaji ikiwemo kuzalisha ajira 2,661 katika mikoa 4 ya Kanda ya Kaskazini kwa mwaka 2021/22.
Akizungumza katika kikao cha Mwongozo wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi Ngazi ya Mkoa na Wilaya kilichoshirikisha wadau wa Baraza la Biashara Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesisitiza kuwa Arusha ni mkoa nyeti katika ukuaji wa uchumi nchini.
Amesema kuwa serikali haina vikwazo kwa mwekezaji yeyote aliyekidhi vigezo vya kupata vibali kwa ajili ya kuwekeza Tanzania
Amesema ni lazima kujipanga kuleta maendeleo kwa wananchi, ikiwemo kukuza sekta mbalimbali kibiashara, ili kukuza uchumi wa nchi, kwani mkoa huo unaongoza zaidi katika sekta ya utalii.
Amesisitiza kikao hicho kiwe na tija ya kuhakikikisha wanatatua changamoto zilizopo kama mkoa katika sekta mbalimbali, ili kuwezesha uchumi kukua ikiwemo ongezeko la ajira
Naye Meneja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kanda ya Kaskazini, Daud Stephano amesema Arusha ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri katika miradi mbalimbali ya uwekezaji kwa Kanda ya Kaskazini.
Amesema Mkoa wa Arusha umeongoza kwa kuwa na miradi 13 kati ya miradi 30 ukifuatiwa na Mkoa wa Tanga 9, Manyara 5 na Kilimanjaro miradi 3.