NAIBU Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde amebainisha kwamba serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kuuwezesha Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 3,304.8 eneo kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima ambalo litafungwa miundombinu ya kisasa ( _centre pivot_)
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Mei 18, 2023 mjini Morogoro aliposhiriki katika maadhimisho ya Siku ya Watumishi wa ASA (ASA FAMILY DAY) ambayo yaliambatana na mafunzo kwa watumishi wapya 141 walioajiriwa na ASA.
“Upatikanaji wa mbegu bora ni eneo muhimu sana katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa chakula.“Amesema na kuongeza
“Ndiyo maana, wote mtakuwa mashahidi, serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya wakala wa mbegu kutoka milioni 500 miaka mitano iliyopita hadi kufikia bilioni 53 mwaka 2023/2024”.Amesema

Amesema, ni matarajio ya serikali kuwa, ongezeko hilo la bajeti katika Taasisi ya mbegu linakwenda kuonekana moja kwa moja kwa wakulima kupitia kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora na hatimaye uzalishaji wa mazao nchini.
“Taifa lolote ambalo lipo huru, lenye kulinda heshima na utu wa watu wake, ni lile ambalo linajitosheleza kwa chakula na uchumi imara.
“Ili uwe na uhakika wa chakula ni lazima kuimarisha uzalishaji, tija na kuwa na umiliki wa mbegu zetu kwani atakayetawala dunia hii ni yule ambaye ana umiliki wa mbegu bora na utoshelevu wa chakula.” Alimnukuu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe
Aidha, amewataka wafanyakazi wa ASA kuwa chachu na hari ili kutekeleze majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu mkubwa huku wakikumbuka jukumu kubwa walilonalo katika Taifa letu.
Awali, akitoa mwelekeo wa Wakala, Afisa Mtendaji Mkuu wa ASA, Dkt. Sophia Kashenge alisisitiza kuwa idadi ya watu duniani inakadiriwa kufikia bilioni 10 ifikapo mwaka 2050, ambapo mahitaji ya chakula yataongezeka maradufu, hivyo ni dhahiri kuwa mbegu bora ni muhimu sana ili kuongeza uzalishaji wa chakula utakaokuwa unaendana na ongezeko la watu duniani.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya ASA ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Marco Mtunga aliwaeleza watumishi wa ASA juu ya umuhimu wa kuthamini na kujali kazi wanayofanya kwani Serikali ina matarajio makubwa sana kwao katika kuinua tasnia ya mbegu nchini.