Asas adokeza majukumu ya mabalozi kuelekea uchaguzi
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimeainisha majukumu ya mabalozi wa chama hicho katika maandilizi yake ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025.
Mabalozi hao 192 wa Iringa Mjini leo wamekutana na kuzungumza na mlezi wa chama hicho Mkoa wa Iringa, Mohamed Aboud Mohamed ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa wakati akihitimisha ziara yake ya siku nne iliyompeleka wilaya zote za Mkoa wa Iringa kujionea maendeleo ya chama hicho.
Akizungumzia umuhimu wa mabalozi hao ambao kwa mujibu wa Katiba ya CCM ndio wenyeviti wa mashina ya chama hicho, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas alisema:
“Mabalozi hawa ambao wengi wao ni wazee wetu wa chama wana jukumu muhimu katika chama chetu. Wao huleta utaalamu, uzoefu, na hekima katika uendeshaji wa chama na ndio maana leo tumeona ukutane nao na uzungumze nao.
Asas alisema wazee hao wanaweza kutoa ushauri kwa viongozi wa chama, kusimamia migogoro, na kuwaunganisha wanachama pale wanapotofautiana.
“Pia, wanaweza kutumika kama wanahistoria wa chama, wakikumbusha misingi na malengo ya awali ya uanzishwaji wa chama hiki. Hivyo, wazee hawa ni nguzo muhimu katika kuhakikisha utulivu na mwelekeo wa chama kwasababu ndio wanaishi na watu huko mitaani,” alisema.
Akiahidi kuwapa ushirikiano, Asas alisema atahakikisha wanafanya nao vikao vya mara kwa mara ili kusikiliza changamoto zao na za Wananchi wao katika maeneo yao.
Akizungumza na mabalozi hao, Mohamed alisema wazee wataendelea kuwa nguzo ya chama hicho ili kiendelee kushika dola na kuliletea taifa na watu wake maendeleo.
“Nia na dhamira ya kwanza ya chama chetu ni kutafuta ushindi. Kwa umadhubuti niliouona, mabalozi na viongozi wa ngazi mbalimbali za chama, madiwani na wabunge nimepata moyo kwamba CCM Mkoa Iringa itaendelea kukipa ushindi mkubwa chama chetu,” alisema.
Aliwataka mabalozi na wana CCM kwa ujumla wao kuendeleza umoja, na kusaidiana na serikali yao kulinda na kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
“Maandalizi ya chaguzi zijazo yanatakiwa kuanza kufanyika sasa ili tukifika wakati wa uchaguzi wenyewe tumalizie kazi ya kukipatia chama chetu ushindi,” alisema.
Awali Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Nancy Nyalusi aliishukuru serikali kwa namna inavyofanikisha utekelezaji wa Ilani yake na kuboresha maisha ya watanzania.
“Serikali ya Mama inatekeleza ahadi zake ili kuwahudumia wananchi na kuboresha maisha yao, imefanya huko nyuma, sasa na itaendelea kufanya hivyo,” alisema Nyalusi huku Mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa kugusia kazi zilizofanywa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, barabara, kilimo, maji na uwekezaji.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin alisema kama vyama vya siasa huchaguliwa na wapiga kura wake kuongoza nchi kwa kuangalia namna vinavyoshughulikia changamoto za wananchi, basi CCM haina kipingamizi cha kuendelea kubaki madarakani.
“Kwa jinsi Dk Samia Suluhu Hassan alivyotekeleza na anavyoendelea kutekeleza Ilani ya CCM hakuna shaka kwamba katika chaguzi zote zijazo tutapata ushindi wa kishindo.” alisema.
Pamoja na kukutana na mabalozi, mlezi huyo wa CCM Mkoa wa Iringa amekutana na kuzungumza na wanachama wa shina namba nne tawi la Mtwivila mjini Iringa.