MFANYABIASHARA na mmiliki wa kampuni za ASAS Group, Salim Abri (ASAS) amejiunga rasmi na uanachama wa maisha wa Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania ‘Red Cross’.
Rais wa Redcross ambaye pia ni Mbunge wa Mufundi, Kusini David Kihenzile, ameiambia HabariLeo kuwa Asas mbali na kujiunga rasmi kuwa mwanachama wa Red Cross, pia amechangia fedha taslimu Sh milioni 5 kwa ajili ya kambi ya vijana wa shirika hilo.
Kihenzile amesema Tanzania Red Cross Society inafanya kazi kwa bidii na kutoa huduma za kibinadamu kwa kufuata kanuni zake saba za ubinadamu, uadilifu, kutopendelea, uhuru, kujitolea, umoja, na kushirikiana kimataifa, hii inaifanya jamii kuiamini na kulisaidia shirika kutimiza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wa Asas, amepongeza Baraza la Vijana na uongozi wote wa Redcross chini ya Rais wake David Kihenzile na kudai kuwa ni kiongozi mwenye maono anatoa matokeo na ameipaisha Redcross kitaifa na kimataifa
Pia amewaahidi vijana kushirikiana nao katika kujenga moyo wa kujitolea kwa Watanzania, kazi ambayo Red Cross wanaifanya.