Asas awa mlezi wa Machinga Tanzania
MFANYABIASHARA Salim Asas kutoka mkoani Iringa leo amekubali kupewa hadhi ya umachinga katika tukio lilikowenda sambamba na kuitikia wito wa kuwa mlezi na mwanachama wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA).
Katika tukio hilo lililofanyika katika soko la Machinga Mlandege mjini Iringa, Asas ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Chama cha Mapinduzi (MNEC) amekabidhiwa kadi, barua ya ulezi, cheti cha pongezi na meza ya kuuzia bidhaa zake za maziwa katika soko hilo.
Hata hivyo meza hiyo pamoja na bidhaa zake aliitoa kwa uongozi wa machinga wilaya ya Iringa huku akiahidi kuwaongezea mtaji katika biashara hiyo ili faida watakayopata iwasaidie kugharamia shughuli mbalimbali za ofisi yao.
Katibu wa SHIUMA Taifa, Venatus Magayane alisema wamempa uanachama huo wakitambua kwamba Asas ni kiongozi wa biashara kubwa mwenye moyo usiochoka wa kutoa ushauri, usaidizi na mitaji kwa wafanyabiashara wadogo.
“Tunakuomba uwe mwanachama lakini pia mlezi wa SHIUMA tukitambua uwezo wako mkubwa katika kukuza ushirikiano na kubadilishana maariafa ya uendeshaji wa biashara hadi kufikia mafanikio makubwa kama yako,” alisema.
Akikubali maombi hayo, Asas ambaye tayari ametoa Sh Milioni 25 kati ya Sh Milioni 50 alizoahidi kwa machinga wa soko hilo kama mtaji watakaoutumia kukopeshana; alitumia tukio hilo kutoa darasa la biashara kwa wafanyabiashara hao.
“Wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo- wote ni wafanyabiashara, kinachotutofautisha ni mitaji tuliyonayo,” alisema.
Hata hivyo alisema changamoto kubwa inayowakabili wafanyabishara wadogo ni dhana waliyonayo ya kutengeneza fedha badala ya kukuza biashara zao.
“Mfanyabiashara mdogo siku zote anafikiria faida anayopata kwa kuuza kiwango kile kile cha biashara anayofanya badala ya kuikuza biashara yake na hivyo kumfanya miaka yote asipige hatua,” alisema.
Alisema kutengeza biashara sio kazi ya lelemama kwani ni jambo linalohitaji uvumilivu, muda na nidhamu kubwa ya fedha.
“Ndio maana awamu ya kwanza ya fedha nilizotoa kwa machinga wa Iringa Mjini, yaani Sh Milioni 25 nilishauri badala ya kuwapa wafanyabiashara hao fedha taslimu kama mitaji, wapewe bidhaa wanazouza ili kulinda biashara zao,” alisema.
Akiahidi kuendelea kuwasaidia wafanyabiashara hao, Asas alisema ni muhimu kwa machinga kukuza uhusiano wenye manufaa katika mazingira yanayoweza kusaidia biashara zao kustawi na kukua sambamba na biashara kubwa.
“Hakuna mtu au taasisi inayoweza kupeleka fedha kwenye vurugu. Nawaomba muwe wamoja kwenye maslai sio maovu. Nipo tayari kufanya makubwa zaidi lakini nitazingatia matendo na mienendo yenu,” alisema.
Alisema atajitahidi kuandaa semina za biashara za mara kwa mara kwa wafanyabiashara hao ili wapate maarifa yatakayokuza biashara zao na kuwafanya katika siku za usoni watoke katika kundi la machinga.
Katika tukio hilo, Asas ameahidi pia kujenga jengo maalumu kwa ajili ya huduma mbalimbali za watoto ambao mama zao wanafanyabiashara katika soko hilo lililojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 200 zilizotolewa na yeye mwenyewe.
Awali Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Gwanda alisema halmashauri yao inazo Sh Milioni 10 zilizotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya machinga ya wilaya na kwamba mpango wao ni kuongeza fedha na kujenga ofisi kubwa zaidi.
“Lakini pia halmashauri yetu ya manispaa ya Iringa ilikwishapitisha mkopo wa Sh Milioni 100 kwa ajili ya Saccos ya Machinga wa Mjini Iringa, kinachosubiriwa ili mpate fedha hizo ni ukamilishaji wa uanzishwaji wa Saccos hiyo,” Ngwada alisema.