ASASI ya kiraia inayofanya uchechemuzi wa haki za kidijitali, demokrasia na uwajibikaji na utawala bora, Jamii Forum imezindua awamu ya tatu ya shindano la habari za kuleta mabadiliko.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa jukwaa hilo, Mexence Melo amesema kuwa katika shindano la msimu huu, linaloanza rasmi Mei Mosi, mwaka huu na kudumu kwa siku 90, litamulika zaidi katika utawala bora na uwajibikaji.
“Katika awamu hii, wananchi wataandika maudhui mbalimbali yanayolenga kuchochea mabadiliko chanya na kupelekea kuwepo kwa Uwajibikaji na Utawala Bora. Katika shindano la mwaka huu, JF itashirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza (SAUT) na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kutambua mchango wao katika upashanaji Habari ikiwa ni Pamoja na kushiriki katika kuwandaa wananchi/vijana waliosomea taaluma ya habari, pia katika kufanya tafiti mbalimbali zinazoleta mabadiliko nchini.
Ili kuweza kushiriki shindano hilo, Melo amesema, mshiriki anapaswa kutayarisha andiko linalochochea mabadiliko na kwenye nyanja zote za Utawala Bora ikiwemo uwajibikaji.
Kwa mujibu wa Melo, andiko linapaswa kuwa kwa lugha ya Kiswahili na linatakiwa kuwa na maneno kati ya 700 na 1,000.
“Matumizi ya picha, vielelezo na video yanaruhusiwa ili kuongezea uzito wa wasilisho. Ikiwa picha/video zilizotumika si za mshiriki, atatakiwa kutaja chanzo. Machapisho yanatakiwa kuwa halisi yasizowahi kuchapishwa sehemu nyingine yoyote. Ubwakuzi (Plagiarism) hautaruhusiwa, amesisitiza.
Hata hivyo Jukwaa hilo limeanisha namna ya kushiriki shindano hilo ambapo mshiriki anapaswa kujisajili kwenye mtandao wa JF na kuwasilisha andiko lake ndani ya siku 90 kuanzia Mei 01, 2023 kupitia jukwaa la “Stories of Change 2023″.
“Ili kushiriki, lazima mtu awe mwanachama aliyejisajili JamiiForums.com ili kuchapisha maudhui yake kwenye jukwaa la shindano la Stories of Change,” amesema.
Katika mpango mkakati wake wa miaka mitano (2020-2024), JF ilidhamiria kuendesha shindano lenye lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki katika kuongeza ubora wa maudhui ya Kiswahili mtandaoni yenye kuchochea mabadiliko kwa kizazi cha sasa na cha baadae.
Awamu ya kwanza ya shindano hili ilifanyika kuanzia Julai hadi Oktoba 2021 ambapo jumla ya wananchi 1,509 walishiriki na kuandika jumla ya machapisho 1,536 huku 936 yakipitishwa kuingia kwenye shindano.
Washindi watano wa kwanza walikabidhiwa zawadi mbalimbali katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Oktoba 2021.
Awamu ya pili ya shindano hili ilifanyika kuanzia Julai mpaka Septemba 2022 ambapo wananchi 1,820 walishiriki na kuandika jumla ya machapisho 2,073 huku 1,462 yakipitishwa kuingia kwenye shindano.
Washindi bora kumi walikabidhiwa zawadi mbalimbali katika hafla iliyofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Novemba 2022.Miongoni mwa maudhui yaliyowasilishwa yamechangia maboresho katika mifumo ya utoaji huduma Serikalini huku baadhi ya taasisi zikipokea mapendekezo na kuahidi kuyafanyia kazi
Hata hivyo, kura za majaji zitabeba asilimia 60 ya ushindi huku kura za wananchi jukwaani zikibeba asilimia 40.
“Washindi watapewa taarifa kuhusu ushindi na akaunti rasmi ya JamiiForums kupitia ujumbe wa faragha katika akaunti zao walizotumia kushiriki na kisha kutangazwa kwenye jukwaa la JamiiForums “Stories of Change” na kurasa za JF katika mitandao ya kijamii (Twitter, Facebook, Instagram na Telegram) na si vinginevyo,” amesema.