ASERI KATANGA: Mtanzania aliyetuzwa na Malkia kwa makubwa anayofanya Afrika

Malkia Elizabeth II akimpongeza Mtanzania Aseri Katanga

‘MCHEZA kwao hutuzwa’ ndio msemo wa Kiswahili unaofaa kumwelezea huyu Mtanzania, Aseri Katanga aliyekaribishwa ndani ya kasri ya Malkia Elizabeth II na kutuzwa kwa mambo makubwa aliyofanya/anayoendelea kufanya ‘nyumbani’.

Katanga ambaye ni mtoto wa saba kuzaliwa katika familia yenye watoto 11 ya Mwalimu Ernest Katumwa na Yuliana Rwegasira, hakufahamu kama inawezekana na yeye akafika ndani ya kasri ya Buckingham.

Baba huyu wa watoto watano aliyezaliwa miaka 64 iliyopita katika Kijiji cha Ishozi Bishura, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, kabla ya kwenda Uingereza mwaka 1979 kwa ajili ya masomo, kusaidia watu wa nchini kwake na Afrika kwa ujumla, ndiko kulikomuweka karibu na familia ya kifalme.

Advertisement

Oktoba 11, 2013, ndipo alipata mwaliko wa Malkia Elizabeth II (marehemu) akimtaka afike kwenye kasri. “Sikuwa na habari yoyote kama inawezekana na mimi kufika ndani ya Buckingham Palace (kasri ya Buckingham),” anasimulia Katanga.

“Ukiona kadi kutoka kwenye kasri, inakuwa shock (mshituko). Sikuamini, nililazimika kupiga simu ili nijue kama ni kweli. Wakaniambia ni kweli. Baada ya kujua ndipo nilianza kujitayarisha,” anasimulia.

Anaendelea kusimulia: “Sasa ukishafika, unaambiwa sababu ya Malkia kukualika. Ulipofika muda, nikiwa nimeshaingia ndani, msaidizi wa malkia alikuja na kuniambia kwamba ndugu Katanga, mtukufu  Malkia yuko tayari kukutana na wewe. Nikaingia ndani na malkia alikuwa ananingoja. Alitoa mkono na mimi nikampa wa kwangu.

Hairuhusiwi kutoa mkono kabla ya yeye kutoa wa kwake. Baada ya kuzungumza naye, alitoa utambulisho kwa Prince Philip (mumewe-sasa marehemu), Prince Charles (sasa Mfalme wa III), Camilla (mke wa Mfalme Charles) na wengine kwenye familia.

Malkia alikuwa amesoma mambo mengi kuhusu mimi, kwa hiyo alikuwa na cha kuongea na mimi…Hupaswi kumuuliza maswali bali mpaka yeye akikuuliza basi unajibu.”

Baada ya tukio hilo la kihistoria kwenye maisha yake, Katanga anasema aliendelea kuwasiliana na kasri ya Buckingham na walitoa idhini ya yeye kutumia picha aliyopiga na Malkia kwenye shughuli za kuendeleza miradi yake. “Lakini hupaswi kutumia picha kwenye mitandao au kwenye mambo ya biashara.”

Kwa kuzingatia ukaribu na familia hiyo ya kifalme, Katanga alikuwa miongoni mwa waombolezaji walioalikwa kwenye mazishi ya Malkia Elizabeth aliyefariki Septemba 8, 2022.

“Nilisikitika sana kwamba malkia niliyekuwa namfahamu hayupo tena… Basi tukafanya mpango tukaenda mpaka Windsor, tukapeleka maua tukajua kwamba hayupo tena,” anasema  Katanga.

Katanga ambaye anaishi katika eneo la Windsor alikozikwa Malkia, anasema alialikwa kwa kuzingatia kanzidata ya kasri yenye watu waliojuana na kiongozi huyo. Hata Prince Phillip alipofariki, Aprili mwaka 2021, anasema pia alikaribishwa.

Taarifa juu ya mambo makubwa aliyofanya zilifikishwa kwa Malkia Elizabeth na aliyekuwa Balozi wa Uingereza nchini, Diana Konakry ambaye aliwahi kufika kijijini kwa Katanga mkoani Kagera.

 Mambo makuu aliyofanya

Ni ukweli ulio wazi kwamba, kama si kazi iliyotukuka aliyofanya na anayoendelea kufanyia jamii Tanzania na Afrika kwa ujumla, Katanga asingepewa tuzo hiyo ya Malkia Elizabeth.

Tuzo iliyotambua mchango wake wa kuwasaidia watoto katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kutokana na kusambaza kompyuta milioni moja kwa watoto katika nchi mbalimbali Afrika ikiwamo Tanzania.

Katanga anaeleza harakati za kusaidia watoto nchini akisema mwaka 1999 alipata bahati ya kukutana na Waziri wa Fedha, wakati huo akiwa Daniel Yona.

Alimwomba wasitoze ushuru kwenye uingizaji wa kompyuta ili waweze kuleta nyingi Tanzania kuwaendeleza watoto upande wa teknolojia ya habari.

“Alinikubalia na huo mpango ulitumika kwa muda wa miaka 11 hivi. Lakini kabla ya hapo, mwaka 1986 nilileta Personal Computer (PC). Nilipofika kiwanja cha ndege, walisema eti PC ilikuwa katika banned items (vifaa visivyoruhusiwa) kuingia Tanzania…Baada ya mashauriano walikubali niingize kwa sababu nilisema bila PC nchi yetu itabaki nyuma.”

Baada ya hapo, Katanga anasema alirudi Uingereza akaanzisha asasi isiyo ya kiserikali iitwayo Computers 4 Africa.

Aliziambia kampuni kadhaa ikiwamo B & Q Plc aliyokuwa akifanyia kazi kama Meneja Biashara, kwamba wanapotaka kubadilisha kompyuta zao wampe azipeleke Tanzania na nchi nyingine zenye uhitaji. “Wengi waliitikia sana. Wakasema ni wazo zuri.”

 

Aseri Katanga akiwa amesimama mbele ya kontena lenye vifaa vya shule alivyotoa kama msaada nchini. 

“Mimi katika yote, nilisukumwa kwamba nikifanya hivi, watoto wengi shuleni na jamii inayowazunguka itafaidika kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Anasema baada ya kuleta kompyuta nyingi Tanzania, alipata wazo kwamba hata nchi nyingine zilikuwa na uhitaji hivyo alianza kupeleka katika nchi nyingine Afrika hususani Sierra Leon na Afrika Kusini.

Anaeleza zaidi kuwa aliweza kufanya hayo yote kwa sababu ya kile anachoeleza kuwa kampuni nyingi za Uingereza, wakitoa kompyuta inakuwa sehemu ya uwajibikaji kwa jamii na ni kwa ajili ya kulinda mazingira hivyo hutoa fedha za kuzisafirisha.

Utoaji kompyuta

Katika kutoa msaada wa kompyuta, vigezo vikubwa alivyozingatia ilikuwa ni shule iwe na umeme na walimu walio tayari kujifunza matumizi ya kompyuta.

“Tuliweza kuwafundisha walimu wengi. Nilikuwa na kituo cha kufundisha walimu pale Makongo High School wakati wa Mwalimu Kipingu (Idd) akiwa Mkuu wa Shule,” anasema Katanga.

“Katika huu mradi, nilifanikiwa kujenga the flagship kwenye kijiji nilipozaliwa, huko Ishozi kwenye Shule ya Sekondari ya Tweyambe. Tuliweza kuweka kompyuta 101 kwenye darasa moja na shule nzima ikaunganishwa kompyuta.”

Chini ya Computer 4 Africa, pia alianzisha kituo cha tehama katika Shule ya Sekondari ya Mandela iliyopo Msata wilayani Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani, baada ya kuombwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

Vitabu, ufadhili watoto

Licha ya kujielekeza kwenye Tehama, Katanga pia amesaidia kuleta kontena nyingi za vitabu vya sayansi kwa kuzingatia uhaba unaokabili nchi. Shule na maktaba nyingi zilipata vitabu hivyo kutoka Uingereza, hasa Wilaya ya Misenyi.

Mambo mengine aliyofanya ni pamoja na kutoa ufadhili kwa watoto wasiojiweza waweze kufikia malengo yao. Anasema watoto wengi wasio na uwezo, wanaweza kufikia kiwango cha juu cha elimu wakisaidiwa.

Ujenzi hosteli

Vilevile Katanga anasema amekuwa akifanya kazi na asasi nyingine kuendesha miradi ya maendeleo nchini. Mfano, kwa ushirikiano na Britain Tanzania Society ambayo yeye ni Ofisa Miradi, wamejenga hosteli ya wasichana mkoani Mara kusaidia watoto waliokimbia kukeketwa.

Chini ya mradi huo, wamesaidia pia kujenga zahanati, choo, visima vya maji na hata kuwanunulia baiskeli wasichana waweze kwenda shule bila matatizo. Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ndiye mlezi wa asasi hiyo.

Kilimo

Aidha, kupitia asasi ya Bukoba Development Foundation (BUDEFO) ambayo Katanga ni Makamu wa Rais, pia amefanya mambo mengi ya maendeleo mkoani Kagera. “Na hii itakuja kuziunganisha NGOs nyingine ili tuweze kufanya vitu vikubwa zaidi mkoani Kagera,” anasema.

Katanga anaeleza kuwa siku hizi anafanya utafiti upande wa kilimo na ufugaji na amewaonesha watu wa vijijini kwamba inawezekana kupata migomba bora isiyokuwa na magonjwa.

Wakati huo huo anawafundisha namna ya kutengeneza chakula asili cha kulisha mifugo na magamba ya migomba kulisha kuku baada ya kuyakata sehemu ndogondogo.

Akieleza siri ya kufanya mambo hayo yote na kufanikiwa, Katanga anasema ni kutokata tamaa. Anatoa mfano kuwa katika kutekeleza mambo hayo, anasema kumekuwapo changamoto za hapa na pale ikiwamo alizokumbana nazo bandarini wakati wa kuleta vifaa vya shule.

Changamoto nyingine ni ya baadhi ya watu kuwa na uelewa mdogo hivyo kutotaka kuona kitu kipya kinaingia kwenye jamii. “Lakini hakuna kukata tamaa kwa sababu unakuwa na wito…”

Tuzo nyingine

Licha ya tuzo ya Malkia, mwaka 2010, Katanga alitunukiwa na Kampuni ya B and Q baada ya kuibuka kuwa mfanyakazi bora wa mwaka miongoni mwa watu 37,000. Anasema alikuwa Mwafrika wa kwanza kupata tuzo hiyo.

Hii ni kampuni ambayo alijiunga nayo baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu na kuajiriwa akiwa Meneja Biashara kabla ya kuanzisha asasi ya Computer 4 Africa.

Sambamba na tuzo ya ufanyakazi bora, kampuni ilimpatia zawadi ya pauni 20,000 na mapumziko ya mwaka mmoja aliyotumia kukaa Tanzania na kuendelea kufanya maendeleo kwa kuanzisha vituo vya kompyuta katika mikoa ya Kagera, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam na Mbeya.

Jambo asilosahau

Katanga ana jambo ambalo katika maisha yake anasema hawezi kulisahau. Licha ya kuwa mzaliwa wa Kijiji cha Ishozi Bishura, Wilaya ya Misenyi na kusoma shule ya msingi hadi sekondari nchini, hasahau siku ambayo watu wa Idara ya Uhamiaji walifika kijijini kwake na kumwambia yeye si mzaliwa wa Tanzania.

Walidai yeye ni raia wa Afrika Kusini. Anasimulia kwamba walichukua hati yake ya kusafiria na kesho yake alikwenda kujieleza. “Baadaye walisema samahani, walipata taarifa zisizo sahihi.”

Kielimu, Katanga alisoma Shule ya Msingi Katano na kisha kujiunga na shule ya kati Mugeza. Alikwenda sekondari ya Kibohehe iliyopo Moshi na alimalizia shule ya sekondari Bukoba. Baada ya kuhitimu kidato cha nne, alikwenda shule ya utabibu Machame.

Mwaka mmoja baadaye alipata ufadhili wa kwenda kusoma Uingereza elimu ya juu baada ya dada zake kumfanyia mpango.

Ndoto zake ilikuwa awe mwalimu kama alivyokuwa baba yake lakini haikuwa hivyo. Anasema amejikuta akiwa mwalimu kwa namna nyingine kwani amekuwa akitoa mihadhara kwenye vyuo vikuu akifundisha vijana namna ya kufuga.

“Nafanya research na universities za Makerere, Kenyatta na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kupitia Bio Innovate Africa,” anasema.

Katanga pamoja na mkewe Dorothy Hope, wamejaliwa watoto watano; Margaret Atugonza, Asimwe, Esebi, Jackson na Dk Jessica Alinda. Miongoni mwa mambo anayopendelea ni pamoja na kutembelea nchi ambazo hajawahi kwenda.

Ushauri kwa diaspora

Mwanadiaspora huyu anasema Tanzania inaweza kupiga maendeleo ya kasi zaidi ikiwa kila mtu atatoa mchango wa mawazo na maono sahihi yakakubalika mpaka ngazi ya juu.

Katanga anasema wapo wana diaspora wengi walio tayari kuchangia nchi endapo vikwazo vitaondolewa. “Diaspora wanataka uraia pacha na si special status (hadhi maalumu) kwa sababu diaspora hawataki kuwa zaidi ya wengine.”

“Wanataka na watoto wao waliozaliwa nje ya nchi nao waje nyumbani wachangie kuleta maendeleo. Hawa vijana wa siku hizi wamesoma kwenye vyuo vikuu vizuri sana, wakipata mwongozo mzuri ni faida kwa nchi ya Tanzania.”

Anasisitiza kuwa diaspora wengi ni wazalendo, wanatuma fedha nyingi nyumbani kusomesha ndugu na jamaa na wanashiriki kazi nyingi za kujitolea kwenye maeneo waliyotoka.

Anasema wanadiaspora wanazungumza na marafiki au wafanyakazi wenzao waje kutembelea Tanzania. Wanajenga nyumba au kulima mashamba hatua inayosaidia kuongeza ajira na mzunguko wa fedha.

Katika makala iliyowahi kuchapishwa katika gazeti la Daily News juu ya Mtanzania huyu, mwandishi Dav Kyungu anamtaja Katanga kuwa ni mfano wa kuigwa kwa makubwa aliyofanyia jamii yake na kumfanya Malkia Elizabeth kumtuza.

 

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *