TANZANIA italeta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuchangia ujenzi wa viwanda endapo itaimarisha sekta ndogo ya mbegu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Uendelezaji wa Kilimo cha Mbogamboga Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk Gabriel Rugalema aliwaambia hayo waandishi wa habari wanaojifunza masuala ya kilimo.
Alisema taasisi inatambua kwamba Tanzania inachukua hatua madhubuti mbalimbali zenye lengo la kupata matokeo chanya katika sekta ya kilimo, lakini mkazo wa kutosha haujawekwa kwenye mbegu.
“Pamoja na juhudi hizi zote madhubuti, lazima mkazo uwekwe katika kuimarisha sekta ndogo ya mbegu. Ni vizuri mbegu ziandaliwe ndani na kuwafikia wakulima kwa wakati ili kukidhi mahitaji yao,” alisema Rugalemana.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa taasisi hiyo, David Sarakikya, alisema mbali ya kufanya tafiti na kuzalisha mbegu taasisi yao pia ni kisima cha maarifa na utaalamu kwa wanafunzi kutoka nje na ndani ya nchi wanaofanya tafiti zao.