Asifu maneno 200 ya Kiswahili kuingizwa Oxford

BARAZA la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limesema uamuzi wa Kamusi ya Oxford kuingiza maneno 200 ya Kiswahili kwenye kamusi hiyo kunaifanya Lugha ya Kiswahili kujitanua zaidi na kuwa ya kimataifa.

Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi alisema hayo Alhamis alipozungumza na HabariLEO.

Mushi alisema jambo hilo lina matokeo makubwa kwa sababu linatoa picha kwamba Lugha ya Kiswahili siyo lugha ndogo kama baadhi ya watu wanavyodhani, bali ni lugha inayojiweza na ina maneno ambayo lugha nyingine duniani zinatamani kuyachota.

“Kwa hiyo kama wanaiona kwenye kamusi nyingine za kimataifa wanaona kumbe Kiswahili nacho ni lugha ya kimataifa. Kwetu sisi ni jambo la fahari kwa sababu tumeendelea kuikuza lugha yetu, tumeendelea kuuza msamiati wake na msamiati wake unazidi kuingia kwenye lugha nyingine,” alisema Mushi.

Alisema Bakita kama wadau wa Kiswahili na taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia Kiswahili, wamelipokea jambo hilo kwa mikono miwili na wanatamani Oxford na kamusi nyingine waendelee kuchukua maneno mengi zaidi.

Pia alisema kampuni hiyo si ngeni kwao kwa kuwa kuna mwaka walikuja kuchukua maneno matano lakini kwa sasa wamechukua maneno mengi na kuyaingiza kwenye kamusi yao.

Kwa mujibu wa Mushi, kwa kuwa Kamusi ya Oxford inasomwa na watu wengi duniani, hivyo Bakita na Tanzania kwa ujumla, kupitia jukwaa hilo la kamusi, watakuwa wanaitangaza Lugha ya Kiswahili kupitia msamiati ulioingizwa kwenye kamusi hiyo.

Alisema kati ya maneno hayo 200, maneno mengi yamechukuliwa kutoka Tanzania yakiwemo chipsi, mamantilie, singeli na kolabo, hivyo ni jambo jema kwa Tanzania kwa sababu mgeni anayetoka nje kuja Tanzania atakuwa anajua akiagiza chipsi ni kitu gani atakachopewa.

Mushi alisema hakuna lugha duniani inayoweza kusimama yenyewe ikatosheleza maneno yake kwa kila kitu, bali kila lugha inachota maneno kwa mwingine kama Kiswahili kilivyochota maneno kwenye Kiingereza na wao sasa wanaanza kuchota maneno mengi kutoka kwenye Kiswahili.

Kuhusu mchakato wa kuyapata na kuyaingiza maneno hayo kwenye kamusi nyingine, alisema kwa kawaida wahusika ndio wanaochagua maneno wanayotaka kwa kuangalia ni maneno yapi yanayotumika zaidi na hayapo kwenye kamusi za pande zote mbili kwa kuwashirikisha wataalamu wenye utamaduni huo wa Kiswahili.

Mushi alisema lengo la wataalamu hao kushirikishwa ni ili waridhie kwamba maneno yaliyochaguliwa yamesanifishwa na yanatumika na kisha kufikia hatua ya kuyaingiza kwenye kamusi ya Kiingereza.

“Kama sisi tunavyochota, hatuchoti maneno yote, tunaangalia yale ambayo tunayahitaji, yale ambayo hatuna na wao ndivyo wanavyoangalia yale ambayo hawana wanachota huku kwetu,” alisema Mushi.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button