MTWARA: Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) mwaka 2022/2023 unaonesha asilimia 29 ya watoto kuanzia umri wa 0 hadi miaka 8 ndio wenye uelekeo sahihi wa ukuaji katika Mkoa wa Mtwara na asilimia 47 Tanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa program jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM), Meneja Miradi kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali ya KIMASI Torai Kibiti amesema tafiti hiyo imeonyesha uwepo wa changamoto kubwa ya malezi, makuzi kwa watoto hao.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye halmashauri ya wilaya ya wilaya ya Mtwara mkoani humo.
Hata hivyo maendeleo ya awali ya mtoto hivyo kupelekea kuanzishwa kwa program hiyo ili kujenga msingi imara wa familia.
Program hiyo ina mlenga mtoto kwenye suala zima la afya, lishe, ulinzi na usalama, fursa za ujifunzaji za awali na malezi yenye mwitiko kwenye halmashauri hiyo.
Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani ambaye pia ni mratibu wa program hiyo, amesema kwa kiasi kikubwa migogoro ya familia inayopelekea wazazi kutengana ni chanzo cha watoto wengi kutokukuwa katika utimilifu.
“Niwaombe tu wazazi kuvumiliana kwenye mapungufu ili kujenga msingi bora wa mtoto”amesema Nyonyani
Ofisa Ustawi wa Jamii kwenye halmashauri hiyo, Asha Lukanga amewataka wataalamu waliopata mafunzo hayo kufanyia kazi kwa vitendo ili kuhakikisha lengo la serikali linatimia katika kuboresha malezi ya mtoto.
Hata hivyo kuhakikisha mtoto anakua vizuri kwenye afya ya kimwili, kiakili, heshima, nidhamu, maadili, ufaulu mzuri wenye hofu na Mungu na wazalendo kwa taifa huku akiiomba jamii kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu hao.