Asilimia 50 misitu yaharibiwa Geita

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Geita wamebainisha kuwa takribani asilimia 50 ya maeneo ya misitu ya hifadhi yameharibiwa hadi sasa kutokana na uvamizi wa shughuli za binadamu.

Meneja wa TFS wilayani Geita, Almas Mggalu ameweka wazi katika hafla ya upandaji miti kwa ushrikiano na Jumuiya ya Wazazi wilayani Geita kuadhimisho ya siku ya misitu duniani.

Amesema uharibifu mkubwa umechangiwa na shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji holelea wa madini huku shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya hifadhi zikidaiwa kuwa ndio sababu kubwa.

“Hivi karibuni sote tunashuhudia mabadiliko, na mabadiliko hayana mipaka, mvua zimeadimika, tunasema tunapanua mashamba ili tuvune lakini kumbe tunafukuza mvua.

“Kwa hiyo sote tuamuke, suala la uhifadhi ni la kwetu sote, lisiwe tu ni la watu wa maliasili, sisi (TFS) peke yetu hatuwezi, kwa sababu eneo ni kubwa sana na sisi peke yetu hatuhimili.

“Likiwa la kwetu sote, kazi yetu kubwa itakuwa ni kutoa ushauri, kwa hiyo hii kazi inabidi tuifanye sote kwa pamoja kwani sisi tunaondehsa shughuli zetu karibu na maeneo ya hifadhi ndio tutafaidika zaidi.”

Amesema TFS imeimarisha uzalishaji wa miche ya miti na ndani ya miaka mitatu (2020/23) imezalisha miche milioni mbili kati yake zaidi ya miche milioni 1.65 imepandwa na kusalia na miche 350,000.

Amesema wilaya ya Geita ina misitu ya hifadhi mitatu, msitu wa Geita wenye hekta 50,800, msitu wa Lwamugasa wenye hekta 28,000, msitu wa hifadhi wa Usindakwe wenye hekta 450.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Geita, Rehema Mtawala amewaomba maofisa wa TFS kuwekeza zaidi katika kutembelea na kukagua misitu badala ya kukaa ofisini ili kukabili tatizo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Geita, Robert Nyamaigoro ameshauri TFS kuandaa kongamano la pamoja la wakulima, wafugaji na wachimbaji wadogo ili kujadili na kuelimishana juu ya uhifadhi wa misitu.

Habari Zifananazo

Back to top button