IMEBAINIKA kuwa idadi kubwa ya wananchi waliopo mkoani Katavi asilimia 50 ni watoto.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko alipozungumza na wanawake katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa wa Katavi iliyofanyika mjini Mpanda.
“Mkoa wetu wa Katavi, watoto wa kuanzia siku 1 mpaka miaka 14 kuna watoto 576,514 sawa na 50% ya watu waliopo ndani ya Mkoa wa Katavi” amesema.
Kupitia kundi hilo kubwa la watoto RC Mrindoko amewataka wanawake mkoani humo kuzingatia wajibu wa malezi bora kwa watoto hao, jambo ambalo litawahakikishia kuendelea kuwa salama na kutojihusisha na ajira za utotoni, makundi ya kihalifu kama damu chafu pamoja na mimba za utotoni.
Amesema kuwa watoto wasipopata malezi bora watatengeneza kizazi kisicho bora siku za usoni.
Aidha,amekemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyoendelea kama ubakaji na ulawiti na kuwataka wazazi kutoa taarifa zinazoashiria matendo hayo mapema kwenye vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema.