Asilimia 7 ya Watanzania wanaugua figo
ASILIMIA saba ya Watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo, Bunge limeelezwa jijini Dodoma leo asubuhi.
Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel ameeleza kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo ulihusishwa na shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Dk Mollel amelazimika kutoa majibu hayo ya Serikali baada ya Mbunge Asia Abdukarimu Halamga (Viti Maalum) kutaka kufahamu hadi sasa hali ya ugonjwa wa figo nchini.
“Mheshimiwa Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi kupima figo mara kwa mara kwani kuchelewa kutambua tatizo la figo madhara yake ni makubwa na gharama ya matibabu yake ni kubwa sana,” Naibu Waziri ametoa wito.
Mapema wiki hii, Serikali ilieleza bungeni kuwa serikali ina mpango wa kupunguza gharama za usafisahi figo kutoka kiasi cha Sh 350,000 hadi Sh90,000.
“Tumebaini badala ya huduma hii kuwa Sh350,000 kuna uwezekano kabisa wa mtu kutibiwa kwa kati ya Sh 90,000 hadi Sh150,000 kwa hiyo tuna mpango wa kushusha gharama hizi,” Dk Mollel aliliambia Bunge.
Kuhusu msamaha wa matibabu hayo, amesema ikiwa mhitaji ana barua kutoka kwa mtendaji wako wa kata basi anaweza kupata msamaha wa gharama za usafishaji wa figo.
Kabla ya kauli hiyo ya Serikali, Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Sabu alihoji maswali ya nyongeza akitaka kujua mambo ya kuzingatia ili mtu wa kipato cha chini aweze kupata msamaha wa matibabu hayo.
Akizungumzia juu ya utaratibu, Dk Mollel amesema endapo mtu akiwa na waraka huo kutoka ngazi ya kata, basi utaratibu wa msamaha unafanyika.
Awali, Naibu Waziri aliwaeleza wabunge kuwa kwa sasa huduma hiyo inapatikana katika hospitali mbalimbali hapa nchini ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali za rufaa za kanda na mikoa pamoja na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma.