Asilimia 76 ya watanzania hawapigi mswaki

ASILIMIA 76.5 ya Watu wazima Tanzania wameoza meno kutokana na kutopiga mswaki.

Akizungumza na HabariLeo leo Novemba 22, 2022, Mkurugenzi Msaidizi wa Kinga na Meno kutoka Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzoba amesema watoto walioza meno nchini ni asilimia 31.1

Amesema sababu kubwa ya tatizo la kulegea, kutoboka na kuoza kwa meno linalowakabili watoto na watu wazima katika jamii ni kutopiga mswaki vizuri ikiwa ni pamoja na matumizi ya sukari iliyosindikwa inayopatikana katika vyakula mbali mbali.

“Kawaida mtu anapaswa kupiga mswaki angalau mara mbili kwa siku, asubuhi anapoamka na usiku anapotaka kulala, sasa watanzania wengi kupiga mswaki inaonekana ni kipengelee, wengi wanapata matatizo ya kinywa kwa kutopiga mswaki.”Amesema

Mkurugenzi Msaidizi wa Kinga na Meno  Dk Baraka Nzoba

Kauli ya Dk Nzoba imekuja baada ya Shirika la Afya Dunia (WHO), kutoa ripoti yake juzi Novemba 20, 2022 inayooneysha karibu nusu ya watu duniani sawa na asilimia 45 au watu bilioni 3.5 wanaugua magonjwa ya kinywa, huku watu 3 kati ya 4 walioathirika wakiishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Kwa mujibu wa WHO magonjwa ya kawaida ya kinywa ni kuoza kwa meno, ugonjwa ya fizi, kupoteza meno na saratani ya mdomo.

Ugonjwa maarufu zaidi duniani wa kinywa ni wa kuoza kwa meno ambao unaathiri takriban watu bilioni 2.5 na wengi hawatibiwi .

Ugonjwa mbaya wa fizi  ndio sababu kuu ya kupoteza meno na unakadiriwa kuathiri watu bilioni 1 duniani kote.  Na takriban visa vipya 380,000 vya saratani ya kinywa hugunduliwa kila mwaka.

Wakati huo huo, Dk Nzoba ameitaka jamii kuzingatia afya ya kinywa hususani wajawazito kwani tatizo la afya ya kinywa linaweza kusababisha mimba kuharibika, kifafa cha mimba na kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo.

Nae, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye maeneo tofauti yanayohusu afya ya kinywa na meno na tasnia zinazoambatana na kada hiyo ili kuboresha afya ya kinywa na meno nchini.

“Serikali imeendelea kuwekeza katika nafasi za mafunzo ya madaktari wa magonjwa ya afya ya kinywa na meno, pia tasnia nyingine ambazo zinaambatana na madaktari wasaidizi, wauguzi, mafundi wa mitambo kwa ajili ya meno (Biomedical Engineers), vifaa tiba vya meno na pia katika kuajiri watumishi” amesema Prof. Ruggajo.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo

Aidha, amesema afya ya kinywa na meno ni muhimu sana na ni tatizo, kwani takwimu zinaonyesha kuwa katika kila watu wazima wanne, watatu wameoza meno, katika kila watoto watatu, mmoja ameoza meno na katika kila watu kumi mmoja anatatizo la fizi.

Prof. Rugajjo pia amesema  kwa hali ilivyo sasa ni hospitali za Mikoa na za juu yake ndizo zinazotoa huduma ya afya na kinywa kwa uhakika lakini matarajio na mipango ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vituo vya afya na hospitali za Halmashauri ziwe zinatoa huduma hiyo ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake Dkt. James Kengia akiongea kwa niaba ya mkurugenzi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema kwa hivi sasa Hospitali 142 za Halmashauri zinatoa huduma ya afya ya kinywa na meno.

Habari Zifananazo

Back to top button