Asilimia 99.99 ya kaya zahesabiwa

Anna Makinda

SERIKALI imesema imefanikisha Sensa ya Watu na Makazi kwa kuhesabu kaya asilimia 99.99 na majengo asilimia 99.87. Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anne Makinda alisema jana kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutoa matokeo rasmi ya sensa ya watu na makazi Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma mbele ya Kamati ya Ushauri wa Kiufundi ya Sensa, Makinda alisema kazi hiyo iliyokwisha juzi imefanyika vizuri.

“Hadi kufikia Septemba 5, 2022 kiwango cha kaya zilizohesabiwa nchi nzima na taarifa za kidemografia, kiuchumi na mazingira yake zimekusanywa kwa asilimia 99.99,” alisema na kuongeza: “Kwa upande wa sensa ya majengo, asilimia 99.87 ya majengo yote nchini yamehesabiwa na taarifa zake zimekusanywa. Kati ya majengo hayo asilimia 100 ya majengo yote yaliyochukuliwa taarifa zake na anuani za makazi zimehakikiwa.” Makinda alisema watumishi wote walioshiriki kwenye kazi hiyo wamelipwa haki zao zote kwa mujibu wa mikataba ya kazi.

Advertisement

Makinda alisema utekelezaji awamu ya pili ya sensa umekamilika na sasa wameingia katika awamu ya tatu inayojumuisha shughuli zote za baada ya kuhesabu watu.

“Shughuli hizo ni pamoja na uchambuzi wa taarifa za sensa, uzinduzi rasmi wa matokeo ya mwanzo ya sensa na usambazaji wa matokeo ya sensa,” alisema.

Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza alisema sensa imefanyika kwa ufanisi mkubwa kwa kutumia wataalamu wa ndani na kwamba hilo ni jambo kubwa la maendeleo na la kujivunia.

Akizungumzia asilimia 0.07 na 0.13 za kaya na majengo kutohesabiwa, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema hakuna nchi duniani inayoweza kuhesabu kaya kwa asilimia 100.

Hata hivyo, alisema asilimia hizo ni ndogo na hazina athari katika kupanga mipango ya nchi.