JESHI la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba, 2022, limepoteza askari sita kwa kuuawa baada ya kushambuliwa na wananchi nyakati tofauti, wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya uhifadhi.
Kamishna wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema hayo Desemba 21,2022 wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, alipotembelea kituo cha hifadhi ya msitu wa Pagale, ambacho kilivamiwa na watu zaidi ya 50 kwa lengo la kutaka kuwadhuru askari wa uhifadhi wa kituo hicho .
Profesa Silayo alisema matukio hayo yametokea kwa nyakati tofauti katika kipindi cha kuanzia Januari 2022 hadi Desemba 2022 katika hifadhi za kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Mashariki.
Alisema askari wa kituo cha hifadhi ya Msitu wa Pagale walivamiwa na kundi la watu zaidi ya 50, kwa lengo la kutaka kuwadhuru na walipowakosa walifanya uharibifu wa mali za serikali na kuiba baadhi ya bidhaa zilizokuwa katika kituo hicho.
Alisema uvumizi huo ulifanyika Desemba 16, mwaka huu, wakati askari walipokuwa wameenda kutekeleza majukumu yao na waliporejea walikuta uharibifu mkubwa umefanyika.
“Tunalaani vikali matukio haya ya uvamizi katika vituo vyetu, ambao umesababisha hasara kubwa kwa serikali, lakini hata kugharimu maisha ya askari wetu sita tangu mwaka huu umeanza pamoja na raia, ambao wamekuwa wakitusaidia katika uhifadhi kusabaishiwa ulemavu wa kudumu,” alisema Profesa Silayo.