Askari aliyetuhumiwa kumchapa mtoto na kumjeruhi aachiwa huru

SIMIYU: Mahakama ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu imemwachia huru askari, Abati Benedicto wa kituo cha Polisi Bariadi ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya kumpiga hadi kumjeruhi mtoto wake mwenye umri wa miaka 7.

Februari 16, 2023 Askari huyo alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka moja la kumpiga kwa fimbo hadi kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili mtoto wake kinyume na kifungu cha 169 A kifungu kidogo cha 1 na cha 2 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Katika hukumu iliyosomwa leo Machi 20, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Caroline Kiliwa amesema mahakama imemwachia huru mtuhumiwa kutokana na vielelezo vya ushahidi vilivyoletwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kushindwa kumtia hatiani.

Advertisement

Hakimu Kiliwa amesema kuwa mmoja wa mashahidi wa upande wa mashtaka alikuwa daktari, ambapo maelezo yake yalieleza kuwa wakati anamtibu mtoto alimkuta na tatizo la upungufu wa damu mwilini, mchafuko wa damu pamoja na kuvimba miguu.

“ Ukimsikiliza Daktari hakuna sehemu yeyote ambayo alisema chanzo cha magonjwa hayo ya mtoto ni kupigwa na Baba yake tena kwa fimbo, lakini mtoto mwenyewe alisema alipigwa mara moja tu, Je tunajiuliza kupigwa mara moja na hayo magonjwa na majeraha yote aliyokuwa nayo mtoto yalisababishwa na kipigo cha Baba yake? tena kwa mara moja?” amesema Hakimu Kiliwa.

Hata hivyo Hakimu huyo amesema kuwa mahakama inamwachia huru mtuhumiwa kwa sababu upande wa mashtaka imeshindwa kuthibitisha pasipokuwa na shaka tuhuma zake.

Hakimu huyo amemwachia huru mtuhumiwa, huku akitoa fursa kwa upande wa mashtaka kuwa wanayo haki ya kukata rufaa.