Askari watakiwa kulinda hifadhi kwa vizazi vijavyo

ASKARI wahifadhi wa wanyamapori wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuhifadhi vyema rasilimali kwa ajili ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Hayo yalisemwa Jumapili na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili, Profesa Eliamani Sedoyeka wakati wa mahafali ya 57 ya Chuo cha Wanyamapori Pasiansi (PWTI) mkoani hapa.

“Ni wakati sasa wahitimu kutumia ujuzi waliopata kwa ajili ya kulinda rasilimali zetu. Kumekuwa na wimbi kubwa la ujangili,” alisema.

Alisema anatambua changamoto iliyopo kuhusu ajira na tatizo la uchache wa nafasi za ajira licha ya wahitimu wengi kuwa na ujuzi wa kutosha.

Naye Mkuu wa chuo hicho, Jeremiah Msigwa alisema wanafunzi waliohitimu ni 388 katika kozi tofauti za usimamizi wa kuongoza watalii na usalama wao, astashahada ya ulinzi wa wanyamapori pamoja na astashahada ya uongozi wa watalii.

Alisema ni wahitimu 22 walioshindwa kumaliza masomo yao kutokana na baadhi yao kuumwa, kufeli masomo yao, utovu wa nidhamu na wengine kupata ajira.

Msigwa alisema chuo chao kinakabiliwa na uhaba wa magari katika kufika kwenye mafunzo ya vitendo. Amewaomba wahitimu kuhakikisha wanajitolea katika maeneo yao.

Alisema katika jitihada za kukuza utalii, chuo kitaongeza kozi ya stashahada ya wanyamapori.

Mmoja ya wahitimu, Sanare Kohole alisema elimu aliyoipata itamsaidia katika utunzaji wa silaha pamoja na kupambana na majangili.

Ameiomba Serikali iwasaidie katika kukarabati Fort Ikoma, eneo ambalo wamekuwa wakijifunza kupitia vitendo.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button