Ataka mashirika ya hiari kuungana kukabili utumikishaji watoto

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela amezitaka Taasisi zisizo za Kiserikali (NGOs) kuungana kudhibiti tabia ya utumikishaji wa watoto hasa kwenye maeneo ya migodini na kusaidia kuokoa uhai na nafasi ya elimu kwa mtoto.

Shigela ametoa maelekezo hayo Jumanne katika Mkutano wa Mwaka wa NGOs mkoani Geita na kueleza tatizo la ajira za watoto linatishia usalama wao.

Alisema ipo haja ya NGOs kwa pamoja kuliangalia tatizo hilo na kuja na suluhisho la kudumu kuweza kuokoa watoto wanaokimbilia migodini na kuwasaidia waendelee na masomo ili kuzalisha wasomi wenye kujitegemea baadaye.

“Unakuta wakati mwingine, watoto wadogo badala ya kwenda kusoma na kunufaika na elimu bila malipo shuleni, lakini watoto wadogo wanatumikishwa kwenye migodi, kwa hiyo sisi asasi za kiraia ni wajibu wetu kufuatilia mambo kama haya.

“Ili tuweze kuyakomesha, watoto wetu wasome, waje kulifaa taifa kwa kazi ambazo zitakuwa zinapatikana ndani ya taifa letu, kwa hiyo nataka niwaombe na kuwasihi kushiriki kikamilifu,” alisema Shigela.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara alizitaka NGOs kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya serikali sambamba na kuwekeza kutatua changamoto za kijamii ili kazi zao ziwe na tija.

Mratibu wa Mradi wa Clarity chini ya Shirika la Kimataifa la Kujitolea (VSO), Redman Mjema alisema wamejitosa kusimamia haki za binadamu na ulinzi wa usalama wa mazingira kwenye maeneo hayo kuondoa utumikishaji wa watoto.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button