Ataka utaratibu kuvuna mazao ya misitu uzingatiwe

WANANCHI wametakiwa kufuata sheria na kanuni za uvunaji wa mazao ya misitu na iwapo watafanyiwa jambo lolote kinyume na utaratibu watoe taarifa kwa mamlaka husika.

Naibu Waziri, Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga (CCM).

Mbunge huyo alitaka kufahamu kauli ya serikali juu ya askari wa misitu wanaopiga na kuwanyang’anya mkaa wananchi.

Akijibu swali hilo, Masanja alisema askari wa uhifadhi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge pamoja na kuzingatia haki za binadamu.

Alisema kwa msingi huo wito ni kwa wananchi kuhakikisha pia wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa za uvunaji wa mazao ya misitu.

Masanja alisema pia endapo kuna uvunjaji wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo, wizara haitasita kuwachukulia hatua watumishi wake wanaohusika na uvunjaji huo wa sheria.

Alisema kumekuwepo na wimbi la uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji na uchomaji wa mkaa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia biashara hiyo na kuwa hali hiyo imesababisha kutoweka kwa kasi kwa maeneo ya misitu na kujitokeza kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Masanja alisema inapotokea mwananchi anasafirisha mazao ya misitu bila kufuata utaratibu, mazao hayo hutaifishwa na serikali na kutoa rai kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu husika.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x