WADAU wa maendeleo, sekta binafsi na watu binafsi wameombwa kuunganisha nguvu kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya ambao wameanza kutumia dawa ya methadol kuwashirikisha kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujipatia kipato.
Imeelezwa kuwa sababu ya waraibu hao kuacha kutumia methadol na kurudia dawa za kulevya ni kutokana na unyanyapaa, changamoto za kiuchumi na kutengwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano ya Zinduka Cup jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Asasi isiyo ya kiserikali ya Kurunzi ya Jamii, Hassan Mbonde alisema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuwainua kiuchumi waraibu waliokubali kuachana na dawa za kulevya na kutumia methadol na kunusuru nguvu kazi inayopotea hususani vijana.
Mbonde alisema kuwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), iko tayari kuwapatia mafunzo ya kilimo cha mbogamboga kwa waraibu watakaoshinda katika mashindano hayo, lengo ni kuwainua kiuchumi na kujipatia kipato cha kila siku.
Alifafanua kuwa jamii hiyo imekuwa ikitengwa na kunyanyapaliwa kwa kuwa wanaonekana hawana thamani hivyo kurudia dawa za kulevya jambo ambalo hurudisha nyuma juhudi za serikali na asasi kuwanasua katika janga hilo.
“Jamii inapaswa kujua kwamba waraibu wanaotumia methadol wakipata usaidizi wanaweza kupata nafuu na kuendelea na maisha yao,” alisema Mbonde.
Aliongeza kuwa mashindano yatawakutanisha waraibu wanaopokea dawa katika vituo vya Mbagala Rangi tatu (Roundtable), Muhimbili, Mwananyamala na Temeke na kwamba wanalenga kufikia makundi yote ikiwemo wanafunzi, wanawake, wasanii na wanamichezo ili kuelimisha madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Karim Masoud maarufu Karapina kutoka taasisi ya Haneo alisema ni jukumu la kila asasi kuisaidia serikali katika kuelimisha jamii athari za matumizi ya dawa za kulevya ili kuwa na vizazi salama.
Alisema kuwa kitendo kinachofanywa na jamii cha kuwatenga waraibu wa dawa za kulevya hakitasaidia kupunguza tatizo badala yake huchochea madhara zaidi.