Atangaza vipaumbele vitano vya mazingira

OFISI ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira katika mwaka wa fedha 2023/24 imepanga kutekeleza vipaumbele vitano kikiwemo cha kusimamia utekelezaji wa mpango kabambe wa hifadhi na usimamizi wa mazingira.

Waziri wa Wizara hiyo, Dk Selemani Jafo amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/24 na Bunge lilijadili na kumwidhinishia bajeti ya Sh bilioni 54.

Dk Jafo alisema kupitia Mpango huo Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022–2032), Ofisi yake itaratibu utekelezaji wa shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika miji na majiji ikiwemo udhibiti wa taka na upandaji miti na kuendelea kuratibu utekelezaji wa programu ya kukijanisha Jiji la Dodoma.

Alisema Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka jana hadi mwaka 2032. Dk Jafo alisema mpango huo unabainisha hatua za kimkakati zinazopaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto za mazingira kwa kuzingatia jiografia na mifumo ikolojia ya maeneo husika.

Katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, alisema shughuli zitatekelezwa katika ngazi tofauti ikiwemo kukuza uelewa kwa jamii kuhusu hifadhi ya mazingira.

Aliyataja mambo mengine yatakayofanyika kuwa ni pamoja na kuimarisha na kuhamasisha ushiriki wa wadau katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira, kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi, kuandaa na kutekeleza programu za kurejesha mifumo ikolojia iliyoharibiwa na kuandaa na kutekeleza mipango ya usimamizi na udhibiti wa taka.

Pia alisema wataimarisha usimamizi na uzingatiaji wa sheria, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za uzalishaji viwandani na kuhamasisha kufanyika kwa tafiti za mazingira na matumizi ya matokeo ya tafiti hizo.

“Mpango Kabambe unaweka msingi wa mipango na bajeti shirikishi ya usimamizi wa mazingira katika ngazi zote. Utekelezaji wa mpango huu ni jukumu la kila sekta katika kuhakikisha kuwa mazingira yetu yanaendelea kulindwa na kurejeshwa katika hali yake kwa maeneo yaliyoathirika,” alisema Dk Jafo.

Alivitaja vipaumbele vingine vitakavyotekelezwa kuwa ni pamoja na kuchukua hatua za kupunguza uharibifu wa mazingira, kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni nchini, kutoa elimu kwa umma kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi na fursa ya biashara ya kaboni, kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.

Dk Jafo alisema kupitia sera na sheria hiyo, watatoa elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya sheria na sera ya mazingira, kuratibu utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira.

“Pia tutaandaa na kutekeleza miongozo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ikiwemo Mpango wa Utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame (2023–2030), kufuatilia utekelezaji wa miongozo ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira ikiwemo Mwongozo wa dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza na Mwongozo wa kelele na mitetemo,” alisema Jafo.

Vipaumbele vingine alivyovitaja ni pamoja na kufanya uchambuzi na kutoa vibali vya taka hatarishi, kufanya tathmini ya athari kwa mazingira, ukaguzi wa mazingira, tathmini ya mazingira kimkakati, kutoa mafunzo kwa wakaguzi na wataalamu wa mazingira kuhusu sheria ya usimamizi wa mazingira na kutoa elimu kuhusu sera na sheria ya usimamizi wa mazingira

Habari Zifananazo

Back to top button