ATCL kuchanja mbuga

Kutanua wigo wa safari zake

KAMPUNI ya Ndege Tanzania(ATCL) inatarajia kupanua huduma zake nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya za ndani na nje ya Afrika ikiwemo kwenye nchi za uarabuni ambazo zimekuwa na utamaduni wa kibiashara na Tanzania.

Haya yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi wakati semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) juzi,

Anazitaja njia hizo mpya kuwa ni Dubai(UAE), Muscat(Oman), London(Uingereza), Accra(Ghana), Lagos(Nigeria), Lilongwe (Malawi) na Juba(Sudan Kusini)

“Kwenye safari ya India na China tunafanya vizuri na tunategemea mambo yatakuwa mazuri pia Dubai na Muscat kutokana na uhusiano wetu wa kiutamaduni na biashara. Pia tunakusudia kurudi Johannesburg(Afrika Kusini) na kuongeza safari za kwenda Kinshasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.”

Akizungumzia mafanikio tangu kufufuliwa na kampuni hiyo mwaka 2016, alisema wateja wameongezeka kutoka 4,000 kwa mwezi hadi 90,000 Juni mwaka 2022.

Amesema pia kiwango cha mizigo kinachosafirishwa na kampuni hiyo kimeongezeka kutoka tani tano kwa mwezi mwaka 2016 hadi tani 300 Juni 2022 na kiwango hicho kinatarajia kuongezeka zaidi pindi ndege ya mizigo itakapowasili nchini mwisho wa mwezi huu.

Kwa upande wa safari za ndani ya nchi, Matindi amesema zimeongezeka kutoka tatu hadi 15 huku za nje ikitoka moja hadi 11 na pia ATCL imeingia ushirikiano na mashirika ya nje kama la Ethiopia, Oman, India, Emirate na Shirika la Ndege la Qatar.

Safari za ndani inazofanya ndege za kampuni hiyo ni za kwenda Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Kilimanjaro, Arusha, Kigoma, Zanzibar, Kigoma, Bukoba, Mpanda, Songea, Iringa na Tabora.

Kwa upande wa safari za nje ni Bujumbura (Burundi), Comoro, Lubumbashi (DRC), Ndola na Lusaka (Zambia), Nairobi (Kenya), Harare (Zimbabwe) na Entebbe (Uganda), Guangzhou (China) na Mumbai nchini India.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Matindi anasema mapato yameongezeka Sh milioni 700 hadi bilioni 30 na kupanua soko lake kutoka asilimia 2.4 mwaka 2016 hadi asilimia 57 kwa Juni mwaka 2022.

Pia imeanzisha karakana ya kuhudumia ndege zake hatua ambayo imesaidia kutoka dola za Marekani 166,400 kama matengenezo yangefanyika nje ya nchi huku idadi ya marubani kutoka 14 mwaka 2016 hadi 106 kwa sasa ambao 105 ni wazawa na mmoja katokea Msumbiji na Wahandisi sasa wapo 129 kutoka 27 mwaka 2016.

Aidha, Matindi anabainisha baadhi ya changamoto ambazo ni gharama kubwa za uendeshaji na madeni ya serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button