ATCL yashindwa kutua Bukoba

NDEGE ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imeshindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera kutokana na hali mbaya ya hewa.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafir wa Anga (TCAA) Hamza Johari amekiri kuwa ATCL imelazimika kurejea Mwanza baada ya kushindwa kutua katika uwanja huo ulioshuhudia ajali mbaya kuwahi kutokea katika siku za hivi karibuni ikihusisha ndege ya abiria.

Ndege ya Precision Air ilianguka katika Ziwa Victoria na kuua watu 19 kati ya 43 waliokuwa ndani ya ndege hiyo Novemba 6 baada ya kushindwa kutua katika uwanja wa Bukoba kutokana na hali mbaya ya hewa. Vyombo vya uchunguzi bado vinachunguza. Baraza la Mawaziri liliagiza kuwa uchunguzi huo uhusishe wataalamu ndani na nje ya nchi kubaini chanzo na kushauri hatua stahiki.

“Ni kweli nimepata taarifa ndege ya Air Tanzania imeshindwa kutua kutokana na hali mbaya ya hewa, kulikuwa na ukungu, mvua, radi na giza uwanja ukawa hauonekani, kwa hiyo rubani akafuta safari na kurudi Mwanza na ametua salama,” amesema.

Johari hakutoa ufafanuzi juu ya hatua ambazo mamlaka inachukua juu ya uwanja huo ambao Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliufunga kwa muda na baadaye kufunguliwa kufuatia uchunguzi wa awali kuonesha haukikuwa na tatizo lolote.

Miongoni mwa abiria waliokuwepo kwenye ndege hiyo ni Mbunge wa Viti Maalum Neema Lugangira “Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba. Safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua.

Nampongeza Rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar. Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba.”Neema Lugangira.

Habari Zifananazo

Back to top button